CV YA KOCHA MPYA WA SIMBA HII HAPA....

WAKATI mashabiki wa Simba wakihesabu saa kabla ya kushuhudia kocha mkuu mpya wa kikosi chao akitua Msimbazi, mabosi wa klabu hiyo wamekuja na sapraizi ya aina yake ya kuwaletea kocha kutoka Hispania ambaye anasifika kwa soka la kampa kampa tena!

Awali ilielezwa Simba ilikuwa ikiwapigia hesabu makocha kutoka Afrika akiwamo Rolani Mokwane wa Afrika Kusini, lakini dau lake likawafanya wachomoea mapema licha ya kushawishiwa na Kocha wa Al Ahly, Pitso Mosimane, kisha kuhamia kwa Lamine N’Diaye kutoka Senegal.

Jina jingine la tatu lililokuwa likipigiwa hesabu ni Muargentina Miguel Angel aliyeinoa Wydad Casablanca na ilionekana ndiye alikuwa akikaribia kutua Msimbazi, kabla ya mabosi hao kubadili gia angani kutokana na kuvutiwa na maufundi ya Mhispania, Pablo Franco aliyekuwa katika Tatu Bora.
Taarifa zikufikie rasmi kuwa huyu ndiye kocha anayekuja kuinoa Simba kuchukua nafasi ya Didier Gomes aliyeachana nayo saa chache baada ya kung’olewa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa bao la ugenini na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Mwanaspoti limehakikishiwa kwamba Pablo aliyekuwa akiinoa klabu ya Ligi Kuu ya Kuwait ya Al-Qadsia anakuja nchini akiwavutia mabosi wa Msimbazi kwa sifa zake zinazolingana kwa kiasi kikubwa na alizokuwa nazo kocha wao wa zamani, Sven Vandenbroeck aliyewafikisha makundi ya CAF msimu uliopita kisha kutimkia FAR Rabat ya Morocco.

Unaambiwa muda wowote kuanzia sasa kocha huyo ambaye majina yake kamili ni Pablo Franco Martín akiwa na umri wa miaka 41 tu atatua nchini kabla Ligi Kuu haijarejea tena baada ya mapumziko ya wiki mbili.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni kwamba kati ya kesho na Jumanne, Pablo atatambulishwa na mabingwa hao wa Bara ambao pia ni wawakilishi pekee wa nchi katika michuano ya kimataifa, ikiwa inashiriki mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba katika kuhakikisha wanakuwa na benchi imara la ufundi, Pablo hatakuja peke yake, ila atakuwa na msaidizi mmoja - mtaalamu wa viungo kuchukua nafasi ya Adel Zrane aliyetemwa sambamba na Gomes na kocha wa makipa, Milton Nienov kutoka Brazili.

“Kila kitu ni kama kimekamilika baada ya Franco (Pablo) kutuma maombi aliingia kwenye makocha watatu bora akiwa na Miguel Angel na Lamine N’Diaye, ila wasifu na gharama zake zilimpa nafasi ya kuwapiku wenzake na sasa anakuja kuinoa Simba,” alisema kiongozi mmoja wa juu.

“Franco (Pablo) alifanya vizuri hata mahojiano na jopo la kutafuta kocha mpya na kila ambacho alitakiwa kukijibu alitoa majibu sahihi. Ndio maana tulimpitisha na sasa tupo katika hatua za mwisho kukamilisha aje nchini na huyo msaidizi wake - kocha wa viungo.”

Kigogo huyo ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini aliongeza: “Tumemtumia mkataba wa awali tayari amesaini na kama si leo (jana) Jumamosi, basi Jumatatu tutamtumia tiketi ya kuja nchini kusaini mkataba wenyewe kisha tutawatangaza pamoja na msaidizi wake.”

FUNDI WA PASI NYINGI
Pablo Franco Martin aliyezaliwa Juni 11, 1980 katika mji wa Madrid, Hispania alianza kucheza soka kabla ya kujitosa kwenye ukocha akifundisha timu mbalimbali Hispania kupitia klabu za Real Madrid akiwa msaidizi wa Zinedine Zidane ‘Zizzou’, Getafe katika La Liga, huku akiwa ni mzoefu kwenye soka barani Ulaya, Asia na Mashariki ya Mbali.

Kocha huyo mwenye wasifu wa maana anajipambanua kupenda soka la kuvutia lenye udambwidambwi mwingi wa pasi nyingi za kwenda mbele na umiliki wa mpira ambao kwa msimu huu Simba umekuwa ukikosekana na kuwatia hasira mashabiki wakiona watani wao Yanga wakiupiga mpira wa aina hiyo katika mechi tano za Ligi Kuu Bara.

Mbali na soka la pasi nyingi, lakini pia ni mtaalamu wa mipira iliyokufa ambapo kwa mashabiki wa Simba wamekosa kuona kwa miaka mingi tangu alipoondoka Dragan Popadic kutoka Yugoslavia (Serbia ya sasa) ambaye aliwafanya wapinzani wa timu yake kuogopa kufanya madhambi au kutoa kona.

KLABU ALIZOPITA
Kama kocha, Pablo alianza kuifanya kazi hiyo 2008 akiinoa Coria kama kocha msaidizi hadi 2009 alipohamia Fuenlabrada akiwa pia ni msaidizi na 2010-2012 alikuwa kocha mkuu wa Santa Eugenia zote za Hispania, kisha 2013-14 alijiunga na Puertoliano na baada ya hapo alienda Getafe B, 2014-15 kabla ya kuwa kocha mkuu katika klabu hiyo 2015 katika La Liga.

Alienda Georgia 2016 kuinoa timu ya Saburtalo Tbilisi kwa mwaka mmoja kabla ya kutimkia China 2017-18 kuifundisha Beijing Sport University akiwa kocha msaidizi.

Msimu wa 2018-2019 alikuwa msaidizi wa Zizzou ndani ya Real Madrid katika La Liga iliyokuwa na mastaa kama Gareth Bale, Karim Benzema, Sergio Ramos, Toni Kroos na wengineo na 2019-2021 alikuwa Kuwait kuinoa Al Qadsia katika Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Kati ya 2000 hadi 2005 alifanya kazi kwenye soka la vijana katika klabu za Real Madrid, Rayop Vallecano na Real Valladolid CF zilizowahi kutamba La Liga.

Mbali na kufundisha soka akiwa na Uefa Pro Licence, lakini jamaa pia ni mtalaamu wa kuchambua mchezo kwa kuuangalia (football analysis) akiwa na shahada ya uzamili, pia ni skauti mzuri wa kunasaka vipaji akiwa na taaluma ya utawala, kitu kilichowakuna mabosi wa Msimbazi kumbeba.

Hata hivyo, hana rekodi nzuri ya mataji kama ilivyokuwa kwa Sven, lakini uwezo wake wa kufundisha na hasa soka lililozoeleka Msimbazi imefanya Pablo awe chaguo la kwanza kwa mabosi wa Simba wakiamini kiu yake ya kusaka mafanikio na hasa kufundisha Afrika kutambeba kuisaidia timu yao.

Aliwahi kutwaa ubingwa na timu ya CD Puertoliano katika Ligi Daraja la Nne Hispania (Tercera División). Mwaka 2016 aliifikisha Saburtalo Tbilisi fainali ya play-off kuwania medali ya shaba na kupoteza mbele ya Dinamo Tbilisi baada ya awali timu hizo kumaliza nafasi ya pili na tatu katika Ligi Kuu ya Georgia.

Mwaka juzi akiwa na Qadsia aliiongoza kubeba ubingwa wa Kuwait Super Cup kwa kuinyoa Al Kuwait kwa bao 1-o, likiwa ndilo taji lake kubwa la karibuni.

MASTAA WAITWA
Katika hatua nyingine juzi Ijumaa mchana mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alilishtukiza benchi la ufundi kwa kuitisha kikao ili kujadiliana na kupeana ratiba nzima kisha mastaa ambao walikuwa mapumziko kuitwa kuanza kujifua.

Kuanzia jana Jumamosi, asubuhi kikosi cha Simba kilianza mazoezi katika Uwanja wa Boko Veterans kwa wale wachezaji waliobaki baada ya wenzao kuitwa timu za taifa na huenda wakaongezwa na wengine kutoka timu ya vijana ili kuanza kunoa makali kabla ya kurudi tena uwanjani Novemba 19.

Kaimu kocha mkuu, Hitimana Thierry alisema wameanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu Bara na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa wamepangwa kuanza nyumbani dhidi ya Red Arrows ya Zambia katika mechi itakayopigwa Novemba 28 kabla ya kurudiana kwao Desemba 5 kuamua kama waende makundi ya michuano hiyo au iungane na Yanga, Azam na Biashara United zilizong’olewa katika hatua tofauti za michuano ya Afrika kwa msimu huu.

“Tunaendelea na ratiba ya mazoezi ili kuweka wachezaji sawa katika hali ya ushindani kama wale ambao wapo katika timu za taifa, ila wakirudi na kukutana pamoja wote wanakuwa tayari kwa ushindani,” alisema Hitimana na kuongeza, anataka ligi ikirudi na hata kama kocha mkuu atakuja wachezaji wawe fiti tayari kwa kuendelea na michuano.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0753 336 000

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.