WAKATI WATU WAKIZIDI KUMLAUMU BOCCO...KIPA MBEYA CITY AANIKA UZEMBE WA MORRISON..

KIPA wa Mbeya City, Deo Munishi amekiri kama staa wa Simba, Bernard Morrison angekuwa makini juzi angemfunga.

Kipa huyo maarufu kama Dida, alisema mchezaji huyo ndiye aliyekuwa machachari zaidi na alikuwa makini sana dhidi yake.

Katika mechi hiyo ambayo Mbeya City walishinda bao 1-0, alimuelezea Morrison ni mchezaji mwenye akili nyingi zenye usumbufu kwa mabeki na makipa na alikiri kuna shuti alilipiga hadi likamshtua.

“Mashuti yote yaliyokuwa yanaelekezwa kwangu yalikuwa makali, ila la Morrison liliyazidi yote, kwanza sikutegemea angepiga eneo hilo, mwili wake ulionyesha kama anatoa pasi, akili yake ikaamua kupiga,” alisema Dida na akaongeza;

“Baada ya shuti lile, lilinifanya muda wote nikae chonjo kumuangalia anataka kufanya nini akiwa na mpira mguuni, jambo linaloweza kuwa hatari zaidi, kwani unapodili na mchezaji mmoja, anaweza akakuadhibu usiyemtegemea,” alisema kipa huyo wa zamani wa Simba, Yanga na Ashanti United. Dida alisema mbali na shuti hilo, Morrison ni mchezaji asiyekata tamaa licha ya kwamba Mbeya City ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0, lakini alipambana hadi dakika ya mwisho.

“Ana kitu cha kuleta chachu ya ushindani, ukiwa na wachezaji wengi kwenye timu wasumbufu uwanjani kama yeye, wapinzani wanaweza wakawa na wakati mgumu zaidi,” alisema kipa huyo aliyewahi kuichezea Mtibwa.

Mbali na hilo, alisema Simba kwa jumla ilicheza mpira mzuri, isipokuwa matokeo ni bahati ambayo iliwaangukia wao.

“Bado wana nafasi ya kufanya vyema, matokeo ndivyo yalivyo, ukifungwa leo kesho unashinda, hiyo ndio maana halisi ya ushindani wa ligi, ila haimaanishi kwa sababu tumewafunga tukaona kikosi chao kibaya siyo kweli,” alisema kipa huyo aliyewahi kutamba na Taifa Stars.

Post a Comment

0 Comments

Close Menu