YANGA YA GSM YAZIDI KUFANYA 'KUFRU' KWENYE SOKA LA BONGO...WATUMIA ZAIDI YA MIL 600 KWA HILI TU..

YANGA hadi sasa imekamilisha usajili wa vifaa vitano katika usajili wa dirisha dogo ikilenga kukiongezea makali zaidi kikosi chake kinachoongoza msimamo wa ligi kikiwa na pointi 29.

Wachezaji hao watano iliyowanasa ni; Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Crispin Ngushi, Denis Nkane, Abuutwalib Mshery na huku ikielezwa ikimsainisha Moses Phiri mkataba wa awali.

Katika kudhihirisha safari hii imeamua kuwa na kikosi cha kibabe, Yanga imeonyesha jeuri mbili ambazo bila shaka zinaweza kuwa zimewashtua wapinzani wao hasa Simba katika dirisha hili dogo la usajili.

Jeuri ya kwanza ya Yanga ni kutumia zaidi ya Sh 600 milioni katika kukamilisha usajili wa nyota hao watano, lakini jambo la pili, katika ya wachezaji hao wote, ni mmoja tu amesajiliwa akiwa mchezaji huru huku wengine wote wakinaswa baada ya Yanga kuvunja mikataba kwenye timu zao.

Ni Sure Boy pekee katika orodha hiyo ambaye amesajiliwa kama mchezaji huru, lakini wengine wanne waliobakia wamejiunga na Yanga baada ya klabu hiyo kumalizana na kulipa fedha kwa timu zao ambazo zimetoa baraka zote kwa nyota hao kutua Jangwani.

Kiungo Sure Boy amejiunga na Yanga kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na Azam lakini hata hivyo usajili wake haukuwa rahisi na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 27, wametumia kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya Sh 70 milioni kumshawishi kiungo huyo fundi.

Ukiondoa huyo, Yanga imelazimika kuvunja benki kwa ajili ya kuzilipa klabu ambazo nyota wake wengine wanne walikuwa wanazichezea lakini pia kwa ajili ya dau binafis la wachezaji hao ili washawishike kujiunga nayo.

Usajili uliochota kiasi kikubwa cha fedha kwa Yanga katika dirisha hili dogo la usajili ni ule wa Moses Phiri ambaye klabu hiyo imedaiwa kutumia zaidi ya Sh 350 milioni kumnasa.

Phiri alisaini Zanaco mkataba wa miaka miwili unaoelekea mwishoni ambao Yanga imeuvunja kwa zaidi ya Sh 200 milioni na kiasi kingine atachukua Phiri mwenyewe kama dau binafsi nje ya mshahara na posho ambazo atapata ndani ya Yanga. Japo taarifa zingine zinasema Zanaco imemgomea Phiri kuondoka sasa klabu hapo hapo hadi mwishoni mwa msimu.

Yanga pia imetumia takribani Sh 40 milioni kufanikisha usajili wa Nkane ambaye alikuwa na mkataba wa miezi sita uliobakia kwenye kikosi cha Biashara United ambayo winga huyo alikuwa akikitumikia.

Kipa Abuutwalib Mshery, usajili wake unatajwa kuigharimu Yanga zaidi ya Sh 80 milioni ambapo kiasi cha Sh 50 milioni kimetumika kuvunja mkataba wake uliobakia wa miaka miwili ndani ya Mtibwa Sugar na kingine kitaenda mfukoni mwa kipa huyo.

Lakini pia Yanga imetumia takribani Sh 40 katika usajili wa Ngushi ambaye alibakiza mkataba wa mwaka mmoja na nusu katika kikosi cha wabishi wa Mbeya Kwanza.

Yanga imelazimika kufanya usajili wa nyota hao watano harakaharaka ili kufanyia kazi mapendekezo ya kocha Nasreddine Nabi ambaye ameshauri kusajiliwa kwa kiungo mmoja mshambuliaji atakaeysaidiana na Feisal Salum, winga mzawa wa kuziba nafasi ya winga mmoja atakayeachwa, mshambuliaji wa kati, kipa wa kusaidiana na Djigui Diarra na pia mchezaji wa kigeni wa kuziba pengo la Yacouba Songne anayeuguza majeraha ya goti.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0753 336 000

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.