FAHAMU MAPITO YA SABAYA KATIKA UTUMISHI WAKE KWENYE CHAMA, SERIKALINI NA KUPAMBANA NA KESI

Lengai Ole Sabaya anaweza kuwa ni mwanasiasa na kiongozi aliyeweka rekodi ya kupitia mapito ya misukosuko mingi husani ya kesi mahakamani akiwa mashtaka mazito ndani ya mufa mfupi.

Hata hivyo, kati ya kesi nne za jinai alizofunguliwa, nyingine, yeye peke yake na nyingine akiunganishwa na washirika wake, amezipangua zote na kubakiza moja iki katika hatua za awali.

Historia ya Sabaya inaanza Desemba 26, 1986 alipozaliwa mkoani Arusha. Baada ya elimu ya msingi na sekondari alisoma shahada ya kwanza ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha St John jijini Dodoma.

Jina lake lilianza kuchomoza katika medani za siasa baada ya kuchaguliwa diwani wa Kata ya Sambasha jijini Arusha mwaka 2015.

Mwaka 2016 alichaguliwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha na Julai 28, 2018 aliteuliwa na Rais wa awamu ya tano, John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya Hai mkoani Kilimanjaro.

Pamoja na kupanda huko ghafla, maisha yake kisiasa na uongozi ndani ya chama na Serikali yamekuwa ya misukosuko ambayo imehusiaha kesi mbalimbali.

Misukosuko hiyo ya kesi ilianza mapema tu baada ya kushika nyadhifa hizo, udiwani na uenyekiti wa UVCCM jijini Arusha.

Kujifanya ofisa usalama

Kesi ya kwanza kumwandama Sabaya Septemba 16, 2016 alipotiwa mbaroni na polisi na kuhojiwa kwa tuhuma za kughushi nyaraka za Serikali (kitambulisho cha ofisa Tsalama wa Taifa) na kujifanya ofisa wa usalama wa Taifa.

Septemba 19, 2016 alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha akidaiwa kuwa Agosti 13 katika Hoteli ya Skyway jijini Arusha, alijifanya mtumishi wa usalama wa Taifa na kujipatia huduma mbalimbali kwa njia ya udanganyifu na kwamba .

Pia alidaiwa kuwa katika muda usiojulikana, alighushi kitambulisho cha usalama wa taifa namba MT 86117 ilhali akijua ni kosa la jinai kufanya hivyo.

Hata hivyo, Desemba 14, 2016, Sabaya aliachiwa huru baada ya Serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kueleza hakuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Muda mfupi baada ya kufutiwa mashtaka hayo, alikamatwa tena na polisi na baadaye tena alipandishwa tena kizimbani mahakamani hapo na kusomewa tena mashtaka yaleyale.

Ilipofika Aprili 26, 2017, kwa mara nyingine Serikali ilimfutia mashtaka ikieleza kuwa shahidi pekee ambaye alipaswa kutoa ushahidi amekwenda masomoni nje ya nchi, na hivyo haingekuwa vema kumsubiria mpaka atakaporudi na kufanya hivyo itakuwa sawa na kumnyanyasa mshtakiwa.

Wakili aliyekuwa anamtetea Sabaya, Charles Adiel alipinga maelezo hayo akidai ombi hilo lilikuwa na nia mbaya kwa mteja wake, akidai kuwa lililenga kutaka kuendelea kumshikilia mteja wake.

Alidai kuwa kwa kuwa tayari upande wa mashtaka ulishawaita mashahidi watatu na siku hiyo walipaswa kuwa na shahidi, basi walitaka kutumia vibaya sheria na mwenendo wa mahakama.

Sabaya alidai hilo lilikuwa ni jaribio la pili kwa Serikali kutokana na kushindwa kuwaita mashaidi wa kueleza nani alizipeleka polisi nyaraka husika (vitambulisho hivyo) kwa kuwa mashahidi waliokuwa wametengenezwa kusema uongo walikuwa wakikataa.

Aprili 28, 2017, Sabaya alifutiwa tena mashtaka, lakini baada ya muda akakamatwa tena.

Kufuatia tukio hilo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo aliwaeleza wanahabari kwamba awali Sabaya alipoachiwa waliendelea na upelelezi wa kesi dhidi yake na kwa kwamba angepelekwa tena mahakamani muda wowote kujibu tuhuma hizo.

Na kweli hajuhudi za kutaka sabaya akibu mashtaka hazikuishia hapo, Agosti 10, 2017 alipandishwa tena kizimbani mahakamani hapo akasomewa mashtaka yaleyale.

Wakili wake Edna Mndeme alidai hiyo ilikuwa ni mara ya nne kwa Sabaya kushtakiwa kwa makosa yaleyale, huku akiwa amefutiwa mashtaka hayo mara tatu.

Hata hivyo, Agosti 30, 2017 kwa mara ya nne aliachiwa huru.

Utumishi serikalini

Licha ya misukosuko hiyo, Julai 28, 2018, Sabaya aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa mkuu wa wilaya ya Hai.

Alitumikia nafasi hiyo licha ya kuwepo malalamiko kadha wa kadha hadi aliposimamishwa kazi na Rais wa sita, Samia Suluhu Hassan Mei 13, 2021 kupisha uchunguzi wa tuhuma za makosa mbalimbali zilizokuwa zikimkabili.

Hatua hiyo ndio ilikuwa mwanzo wa utumishi wake katika nafasi hiyo kukoma, kwa kuwa baada ya uchungizi alifunguliwa kesi mfululizo za unyang’anyi, uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya madaraka.

Mei 27, 2021, Sabaya alitiwa mbaroni na polisi Kinondoni jijini Dar es Salaam kisha akapelekwa katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) ambako alihojiwa kwa siku nane kwa tuhuma mbalimbali.Baadaye alisafirishwa kupelekwa jijini Arusha kisha .

Juni 4, 2021: Sabaya na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha wakikabiliwa na kesi mbili tofauti na kwa mahakimu wawili tofauti.

Kesi ya kwanza ya jinai namba 105 ya mwaka 2021 ilikuwa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, yeye na wenzake wawili huku menzake Sylivester Nyegu maarufu Kicheche na Daniel Mbura wakikabiliwa na makosa mawili ya ujambazi wa kutumia silaha, waliyodaiwa kuyatenda Februari 9, 2021

Kesi ya pili ilikuwa ni ya uhujumu uchumi, namba 27 ya mwaka 2021, iliyokuwa ikimkabili na wenzake watano, Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matano yakiwemo ya rushwa mawili na moja la matumizi mabaya ya madaraka. Mengine ya kuunda genge la uhalifu na utakatishaji fedha.

Oktoba 15, 2021, Sabaya, wenzake walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa ujambazi. Hata hivyo, walikata rufaa Mahakama Kuu kuipinga hukumu hiyo.

Mei 6, 2022, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliwafutia hatia na kuamuru waachiwe huru baada ya kushinda rufaa yao. Hata hivyo wakiendelea kuwa ndani kutokana na kuwa na kesi nyingine.

Mei 30, 2022, Serikali ilimfungulia kesi nyingine ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoa wa Kilimanjaro, mjini Moshi.

Juni mosi, 2022 yeye na wenzake wanne Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antoro Assey walipandishwa kizimbani mahakamani hapo katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi uchumi namba 2 ya mwaka 2022.

Walisomewa mashtaka saba, ya rushwa mawili, ukiukwaji ya utumishi wa umma moja (kwa Sabaya pekee); kuongoza genge uhalifu na utakatishaji fedha (kwa wote), mashtaka mawili kumsaidia Sabaya kushawishi na kujipatia manufaa asiyostahili ya Sh30 milioni (kwa wenzake).

Juni 10, 2022, Sabaya na wenzake sita walipangua kesi ya pili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha, baada ya kuwaona kuwa hawana hatia.

Mahakama hiyo ilisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka yoyote, ikieleza ilichokieleza kuwa ushahidi wake uligubikwa na utata na kwamba hati ya mashitaka ilikuwa na upungufu wa kisheria.

Kwa hiyo, kwa sasa Sabaya amebakiza kesi moja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Kilimanjaro, mjini Moshi inayomkabili yeye na wenzake.

Je, ataweza kukiruka na kiunzi hicho? Tusubiri.

Chanzo - Mwananchi

Post a Comment

0 Comments

Close Menu