WAUMINI KKKT WAMPONGEZA MCHUNGAJI NKYA KWA UTUMISHI WAKE

Waumini wa Kanisa La Kiinjili La Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu mjini Shinyanga wamempongeza aliyekuwa msaidizi wa askofu wa kwanza wa Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria na Dean wa usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Shinyanga mchungaji Trafaina Assery Nkya kwa utumishi wake wa uchungaji katika kanisa hilo.

Waumini hao kwa umoja wao wametoa pongezi hizo katika ibada ya Jumapili ya tarehe 12/06/2022.

Akieleza juu ya utumishi wa Mchungaji Nkya, Askofu wa Dayosisi hiyo Mchungaji Daktari Emmanuel Joseph Makala alisema kuwa kwa kipindi chote cha utumishi wake Mchungaji Trafaina Nkya ameshinda mengi.

 "Hadi kufikia hatua ya kustaafu na kwa jinsi ninavyomfahamu Mchungaji Nkya simung'unyi maneno ila tu niseme kuwa huyu baba ameshinda mengi. Unapokuwa mkubwa (Askofu/msaidizi wa askofu), wewe unakuwa mtu wa kuletewa yale mambo mabaya tu na yale mazuri huletewi isipokuwa yanaishia tu kule chini, hivyo jambo la kufikia hatua hii lazima unakuwa umeyashinda mengi. Kwa hiyo mchungaji nikupongeze sana kwa utumishi wako kwa kanisa la Mungu" alisema Askofu Makala

Kwa upande wake msaidizi wa askofu mstaafu mchungaji Trafaina Nkya, ameshukuru sana kwa tukio hilo lililofanywa na washarika wa usharika huo kwani wameonesha upendo mkubwa sana kwake. 

"Awali ya yote nimshukuru sana Mungu kwa siku ya leo, nikushukuru Baba Askofu Emmanuel Makala kwa kuruhusu jambo hili katika usharika wetu, vilevile niwashukuru washarika wote kwa jambo hili ambalo sikulitegemea kabisa kama litafanyika kwa kiwango kikubwa namna hii. Mungu wa mbinguni awabariki sana".

Akisimulia kuhusu utumishi wake katika usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu, Mchungaji Nkaya alisema kuwa baada ya kubarikiwa uchungaji, usharika wake wa kwanza kuanza kutumika ni usharika huu aliopangiwa  mwaka 2001.

"Mimi na wengine tulipangiwa vituo vya kazi tukiwa bado chuo cha theolojia, hivyo wakati nabarikiwa uchungaji siku hiyo hiyo nilikabidhiwa kwa Mzee Gabriel Shoo (msharika wa Shinyanga mjini) tayari kwa kuja kuripoti" alisema mchungaji Nkya

Akielezea changamoto aliyoanza nayo katika usharika huo, mchungaji Nkya alisema juu ya kudharauliwa na miongoni mwa washarika kutokana na kuwa na mwili mdogo mdogo kipindi hicho.

"Nilipofika tu nilidharaulika na wengi kutokana na nilivyokuwa mdogo mdogo hadi kusemewa maneno mabaya na ya kukatisha tamaa. Kwa masikio yangu nilisikia wazi wazi watu wakiambizana kuwa huyu ataweza nini? Mfupa alioushindwa fisi mbwa atauweza?" Alisema Mchungaji Nkya 

Naye msaidizi wa Askofu wa sasa Mchungaji Daktari Yohana Emmanuel Nzelu, alisema kuwa Mchungaji Trafaina Assery Nkya kwake amekuwa ni mzee toka enzi na enzi. Tangu akiwa mwinjilisti wake katika usharika wa Imani Kanisa Kuu Mwanza uliopo Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria 

"Baba msaidizi wa askofu mstaafu mchungaji Trafaina Assery Nkya, nakupongeza sana mzee kwa utumishi wako mwema na uliotukuka ndani ya shamba la Mungu. 

"Wapendwa washarika, kwangu mimi nimekuwa nikijifunza mambo mengi sana kupitia kwa kwa huyu mzee, na nimekuwa nikimwita mzee siku nyingi tangu akiwa mwinjilisti wangu katika usharika wa Imani jijini Mwanza nami nikiwa Mwenyekiti wa kwaya kipindi hicho."

"Amekuwa ni mtu wa kunishauri kwa kipindi chote tangu nimfahamu, na hata sasa tangu astaafu bado ameendelea kunisaidia na kunishauri kwa masuala yote ya kiofisi kama mtangulizi wangu" Alisema Nzelu

Akielezea juu ya utumishi wa mchungaji Nkya, Chaplain wa Kanisa Kuu mchungaji Odolous Gyunda alisema kuwa kwa sehemu kubwa ya utumishi wa Mchungaji Nkya washarika wa usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Shinyanga ndio wameufaidi kuliko sehemu nyingine yoyote ile

"Mimi niseme wazi, hata siku ya kwanza wakati natangaza kuhusu kumpongeza huyu baba, washarika mtakumbuka niliwaambia kuwa kama kuna watu wamefaidi utumishi wa huyu mzee ni washarika wa usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu, na kama kuna watu ambao wamemfanya huyu baba aumie au afurahi ni washarika wa Ebenezer Kanisa Kuu"

"Hivyo nikisema kuwa asilimia zaidi ya 90 ya utumishi wa Mchungaji Nkya umekuwa ni hapa Ebenezer". Alisema Odolous 

Mchungaji Nkya alikuja usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Shinyanga mwaka 2001 ukiwa unajulikana kama usharika wa Shinyanga mjini. Mwaka 2011 alihamishiwa usharika wa Efeso uliopo ndani ya mgodi wa Mwadui Kishapu Shinyanga na mwaka 2012 alirudishwa tena usharika wa Ebenezer Shinyanga akiwa kama msaidizi wa askofu na Dean wa Kanisa kuu.

Mchungaji Nkya atakumbukwa kwa utumishi wake mwema kwa KKKT hususani katika usharika wa Ebenezer Shinyanga na dayosisi kwa ujumla.  Atakumbukwa kwa mambo mengi aliyoyafanya ikiwemo kufungua sharika nyingi ndani ya Mkoa wa Shinyanga na maono ya ujenzi wa jengo la kuabudia katika usharika huo.

Mchungaji Trafaina Nkya akiwa na Askofu Emmanuel Joseph Makala mara baada ya ibada ya kupongezwa kwake.
Katibu mkuu wa Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria Bi Happines Gefi akisema neno  wakati wa ibada ya kumpongeza mchungaji Nkya.Isaac Masengwa - MASENGWA BLOG

Post a Comment

0 Comments

Close Menu