MWANAFUNZI wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Usule, Kata ya Usule, Halmashauri ya Shinyanga mwenye umri wa miaka 17 (jina limehifadhiwa), anadaiwa kutoroshwa na mganga wa jadi aliyetokea Tanga na kwenda naye kusikojulikana.
Imedaiwa kuwa mganga huyo alifika kwenye kata hiyo kuwaogesha dawa za mvuto wa mapenzi maarufu ‘samba’ wanafunzi na mabinti walio katika umri wa balehe ili wapate wanaume wa kuwaoa kwa kuwashirikisha wazazi wao.
Mratibu wa mradi wa Tuwawezeshe kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Rafiki-Sdo, mkoani Shinyanga, Maria Maduhu, aliyabainisha hayo jana wakati akitoa taarifa ya tathmini ya ufungaji wa mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, uliofadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT).
Alisema wakati wa utekelezaji wa mradi huo, walikutana na visa viwili vikubwa vilivyowashirikisha wazazi, kikiwamo cha watoto kuogeshwa dawa na mganga na kutoroka na mwanafunzi huyo.
Aidha, alidai kuwa kisa cha pili ni cha mwanafunzi wa Kata ya Ilole, aliyeogeshwa dawa hizo na kupata mwanaume wa kumuoa na baada ya siku kadhaa ndoa ilivunjika na mwanafunzi huyo kubainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Alisema walifanikiwa kuwafikia zaidi ya wananchi 263 katika kata za Ilole na Usule na kuwapatia elimu ya mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE, John Myola, alidai kuwa waganga wa jadi wanawahadaa wazazi kuwa baada ya mtoto kuogeshwa dawa za mvuto wa mapenzi mwanaume yeyote atayekutana naye barabarani na kumsemesha atakuwa mume wake.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Deus Mhoja, alisema matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake bado yapo juu katika halmashauri hiyo na kwamba wataendelea kupambana ili kuhakikisha yanakwisha kabisa.
Alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023, halmashauri hiyo imetenga Sh. milioni 21 kwa ajili ya kuendeleza mabaraza ya watoto, majukwaa ya wanawake katika kata zote.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mfuko wa Wanawake mkoani Shinyanga, Glory Mbia, aliiomba serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kupambana na ukatili wa kijinsia katika jamii ili kuwapatia fursa wasichana kuendelea na masomo yao.