KUNDI la nyuki ambalo halikujulikana limetokea wapi limezua taharuki baada ya kuvamia Shule ya Msingi ya Kamena Wilaya ya Liwale mkoani Lindi na kujeruhi walimu na wanafunzi.
Taarifa kutoka wilayani humo na kuthibitishwa na mmoja wa walimu wa shule hiyo, Rehema Mwaitenda, zinaeleza tukio hilo lilitokea saa nane mchana, Julai 26, mwaka huu.
Mwaitenda alisema siku ya tukio, yeye na walimu wenzake wakiwa wanaendelea na majukumu yao ya kikazi, kundi hilo la nyuki lilivamia shuleni hapo na kuwashambulia walimu na wanafunzi.
Alisema katika uvamizi huo, wanafunzi wanane pamoja na walimu wawili walikimbizwa Hospitali ya Wilaya mjini Liwale na kupatiwa matibabu baada ya kung’atwa na nyuki hao.
“Katika uvamizi ule wanafunzi wanne walilazimika kupumzishwa wodini kutokana na maumivu makali,” alisema mwalimu huyo.
Mmoja wa wauguzi katika hospitali hiyo, ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa sio msemaji wa hospitali, alithibitisha kuwapokea majeruhi hao na kueleza kuwa walitibiwa na kuruhusiwa kurejea majumbani mwao, huku wanafunzi wanne wakalazimika kupumzishwa kwa muda.
“Ni kweli juzi tuliwapokea majeruhi wasiopungua kumi, wakiwamo walimu wawili na wanafunzi wanane,” alisema.
Hata hivyo mmiliki wa shule hiyo hakupatikana kuzungumzia tatizo hilo na haikufahamika mara moja iwapo nyuki hao walitokea wapi.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Noel Manyasa, akizungumza na Nipashe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanafunzi wanaendelea vizuri.
“Tuliwaita watu wa maliasili wakawafukuza nyuki hao, lakini mti waliokuwa wametua kwa wingi tuliukata ili kutowavutia kurudi,” alisema.
Aidha, alisema wanafunzi wanane na walimu wawili walijeruhiwa wakalazwa Hospitali ya Wilaya ya Liwale kwa matibabu zaidi na kwamba hali zao zinaendelea vizuri huku wanafunzi wanne wakipewa mapumziko.