Kwa sasa, Andrey akishirikiana na wataalamu na wanazuoni wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini, wanaendelea na hatua za mwisho za usanifu na uboreshaji wa huduma hiyo, kabla ya kuanza kutumika kikamilifu.
SHULE YASIMAMIA UBORA WA ELIMU NA TEKNOLOJIA
Akizungumzia safari ya miaka minane na mafanikio ya taasisi hiyo, Mkurugenzi wa Abel Memorial Pre and Primary School, Mhandisi Stanslaus Abel Mwalongo, alisema moja ya mafanikio makubwa ya shule hiyo ni kufanya vizuri katika taaluma.
Alisema wanafunzi wengi waliohitimu katika shule hiyo wameendelea na masomo katika shule mbalimbali zenye ushindani mkubwa, jambo analolitaja kuwa ni sehemu ya matokeo ya uwekezaji unaofanywa katika elimu na malezi ya wanafunzi.
“Kwa sasa shule yetu inalenga kuendelea kuboresha kitengo cha TEHAMA kwa kuongeza kompyuta za kisasa ili kuwajengea wanafunzi uwezo unaoendana na kasi ya teknolojia ya kidijitali,” alisema Mhandisi Mwalongo.
Aidha, alisema shule ina mipango ya kuendelea kuboresha miundombinu yake, ikiwemo ujenzi wa mabweni, yatakayowawezesha wanafunzi wa madarasa yenye mitihani kukaa shuleni na kupata muda zaidi wa kujisomea, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na matokeo ya kitaaluma.
WANAFUNZI WAONESHA UBUNIFU WA HALI YA JUU
Katika maadhimisho hayo, wanafunzi walipata fursa ya kuonesha vipaji, maarifa na ujuzi walioupata shuleni kupitia maonyesho mbalimbali yaliyohusisha lugha, hesabu, sayansi na TEHAMA.
Kilichovutia zaidi ni namna wanafunzi walivyowasilisha maarifa hayo kwa vitendo, jambo lililoonesha kuwa Abel Memorial Pre and Primary School si mahali pa kujifunza nadharia pekee, bali pia ni mazingira yanayowajenga watoto kuwa wabunifu, wenye kujiamini na wanaoweza kutumia elimu kutatua changamoto zinazowazunguka.
Maonyesho hayo pia yalitoa picha ya mazingira ya shule yanayowapa wanafunzi nafasi ya kufikiri kwa uhuru, kuhoji, kubuni na kuonesha vipaji vyao tangu wakiwa katika ngazi za awali za elimu.
PADRI ATOA WITO KWA WAZAZI
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na ibada takatifu iliyoongozwa na Padri Paul Malewa wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmel Bunju, Jimbo la Bagamoyo, ambaye alisisitiza umuhimu wa wazazi kushirikiana na shule katika kuwalea watoto wenye nidhamu, uwajibikaji na uwezo wa kujitegemea.
Padri Malewa aliwataka wazazi kuepuka kuwalea watoto kwa kuwazoesha kutegemea kila kitu kufanyiwa, badala yake wawajengee uwezo wa kujitegemea tangu wakiwa wadogo.
“Ni vema wazazi wakawafundisha watoto kujitegemea badala ya kuwa tegemezi. Wafundisheni watoto kazi kama kufua nguo zao wenyewe na kupika, badala ya kutegemea mtu mwingine kufanya kila kitu kwa ajili yao,” alisisitiza Padri Malewa.
WAGENI ZAIDI YA 300 WASHIRIKI
Katika mahafali hayo, wageni zaidi ya 300 walihudhuria na kupata fursa ya kushuhudia shughuli mbalimbali zilizofanywa na wanafunzi, pamoja na kupata elimu kuhusu fursa za uwekezaji kupitia UTT, ambayo ilikuwa miongoni mwa wadhamini wakuu wa hafla hiyo.
Kwa ujumla, maadhimisho ya miaka minane ya Abel Memorial Pre and Primary School yamekuwa zaidi ya kusherehekea safari ya taasisi hiyo; yamekuwa jukwaa la kuonesha matokeo ya uwekezaji katika elimu, ubunifu wa watoto, matumizi ya teknolojia na malezi yanayolenga kumwandaa mtoto kwa dunia ya kisasa.
Kupitia mchanganyiko wa mazingira bora ya kujifunzia, msisitizo katika taaluma, ubunifu, sayansi na teknolojia pamoja na malezi, Abel Memorial Pre and Primary School inaendelea kujenga taswira ya shule inayolenga kumwandaa mwanafunzi si kwa mitihani pekee, bali pia kwa maisha na changamoto za kizazi cha kidijitali.
Dirisha la Usajili lipo wazi, kwa Mawasiliano piga simu namba :0784824980

0 Comments