Mbunge
wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameonya kuwa endapo chama hicho hakitataka
kuambiwa ukweli na kukosolewa, utakuwa mwanzo wa kuanguka kwake.
Nape aliyewahi kuwa katibu wa itikadi na
uenezi wa chama hicho, amesema endapo CCM itaua utamaduni wa kukosoana
kupitia vikao itapoteza mwelekeo.
“Hiki chama tukifika mahali tukaanza kufanyiana unafiki kwamba hatutaki
kuambiana ukweli tunapokosea utakuwa ndiyo mwanzo wa kuanguka kwa CCM.”
Amesema hayo juzi nyumbani kwake eneo la Kisasa mjini Dodoma katika mazungumzo maalumu na Mwananchi.
Nape ambaye leo anatimiza miaka 40 ya kuzaliwa, ameeleza kusikitishwa na
namna ya baadhi ya watu aliowaita “vijana wa CCM”, kupotosha kwa
makusudi kauli na ujumbe wake anaoutuma kupitia mitandao ya Twitter na
Instagram.
“Kuna ambao wanamchukia tu Nape kwa sababu wanadhani alishiriki kuzuia
wagombea wao na hasa hawa vijana wafuasi wa Edward Lowassa ambao bahati
mbaya alipohama hawakuhama naye,” alisema.
“Hawa nao wako wanapitia humo kusema hasira zao. Mara Nape huyu anamsema
Rais. Unamuona Nape huyu anaisema Serikali. Hawa nao tuwapuuze. Wakikua
wataacha.
“Wanaona Nape ni beki mzuri wa kufanyia mazoezi au ya kuonekana wapo ili
tu wapewe vyeo. Bahati nzuri mimi nimekulia ndani ya CCM najua lipi
zuri na lipi baya kwa CCM,” alisema.
Mbunge huyo alisema husikitika anaposoma namna kauli zake
zinavyopotoshwa, huku wengine wakidai anatumia maneno makali kwa vile
ameondolewa kwenye uwaziri alikokuwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo.
Nape alisema, “Hakuna jambo ambalo nimelisema kwenye Twitter na
Instagram ambalo halifai kusemwa. Wakati mwingine nina maneno magumu
kwenye vikao. Ninaamini kwenye hayo maneno magumu ndiko ambako
tutakijenga chama chetu,” alisema.
Alisema akiwa katibu wa itikadi na uenezi kuna vikao vilifanyika mpaka
saa sita usiku na alikuwa mkorofi kidogo kwa sababu maneno yake wakati
mwingine yalikuwa magumu.
“Namshukuru sana Kikwete (Rais mstaafu Jakaya) amenilea na amenivumilia
wakati mwingine, maana sarakasi nyingine na ujana huu amenivumilia
sana,” alisema.
Alisema, “Katika watu wenye moyo wa ajabu sana ni Rais Kikwete
(mstaafu). Katibu mkuu wetu (Abdulrahman) Kinana naye ameni shape
(nijenga) sana kunivusha kutoka ujana hadi kukomaa.
“Lakini nasema lazima CCM ijenge utamaduni wa kukosoana na kujikosoa ili
tuende mbele. Tukiua huo utamaduni tutakifanya hiki chama kitapoteza
mwelekeo. Tuujenge kwa nguvu kubwa.”
Akizungumzia aina ya maneno anayoyatumia kufikisha ujumbe kupitia
Tweeter, Nape alisema ujumbe mzuri ni ule ambao ukiwekwa unafikirisha na
unamfanya mtu kueleza namna alivyouelewa.
“Tweet nzuri ni ile ambayo ukiiweka inafikirisha. Tweet nzuri ya mtu
aliyetumia akili, ya mtu msomi huweki tweet ambayo kila mtu akisoma
umeandika shikamoo baba. Inatakiwa iwe ambayo mtu akisoma anafikiria na
anapata hamu ya kuitafakari. Nafurahi sana kwa sababu Tweet zangu
zinasumbua akili wakati mwingine wanapata majibu tofauti tofauti.
“Wengine wananitukana wengine wananituhumu. Kwenye Tweet zangu hizi kwa
sehemu kubwa watu wanapotosha na wanaopotosha wamegawanyika katika
makundi mawili. Kuna ambao hawamjui Nape na hao ndiyo wale wanaosema
Nape toka (tangu) ametoka uwaziri ana tweet hivi lakini nimekuwa
nikiwauliza kwani kabla sijawa waziri, sijawa katibu mwenezi sikuwa
nasema?”
“Wanasahau mimi niliwahi kumnyoonyeshea kidole waziri mkuu wa Tanzania
hadharani nikasema wewe fisadi. Leo wanasema Nape anasema maneno makali
sana! Hivi kuna maneno makali zaidi ya kumnyooshea waziri mkuu wa nchi
ukasema hapa kwenye mradi huu umefanya ufisadi?
“Hawajui mimi ndiye niliyesimama Songea nikasema Kikwete kuna mawaziri
wako hapa ni mizigo. Hivi kuna kauli kubwa ya kufikia hapo?
“Mtakumbuka niliwahi kusimama kwenye mkutano wa hadhara lakini
mtakumbuka nilikwenda Arusha nikamwambia Lazaro (Nyalandu) nenda
katimize wajibu wako acha kuweka watetezi”.
Afikiria kujitoa mitandao ya kijamii
Akizungumzia mkanganyiko wa namna watu wanavyopotosha ujumbe mbalimbali,
Nape alisema, “Pengine nitoke kwenye social media (mitandao ya kijamii)
sababu unaona kila mara uki-post (kutuma) jambo ooh linakuwa kubwa
sana.
“Tena wakati mwingine ni jambo la utani sana. Kwa mfano siku moja
nimeangalia kipindi kwenye televisheni wanasema mara paap na mimi
nikaweka mara paap.
“Nilipoweka mara paap, wakaanza mara paap kahama CCM mara paap kafanya
hivi, unakaa unasema kwa nini wanafikiria negative (mabaya) kwa nini
hawafikirii positive (mazuri)?”
“Kwa nini hawasemi mara paap ameimarisha chama... Ukiyaona haya naanza
kutafakari seriously (makini) umefika wakati nisimame kidogo hii social
media.”
Hata hivyo alisema anaona akifanya hivyo atawapoteza wafuasi wake zaidi
ya 200,000 walioko Tweeter na maelfu walioko Instagram na ndiyo maana
anajiuliza kwa nini atoke kwa sababu ya wapuuzi wachache?
Mbunge huyo wa Mtama alisema pamoja na watu kutafsiri tofauti na
kupotosha maana halisi ya ujumbe wake, hajawahi kuitwa na chama chake
kuhojiwa.
“CCM ni chama kikubwa sana na mimi nimekaa humu zaidi ya miaka 10 nikiwa
mtumishi ukiacha miaka 20 nikiwa mwanachama. CCM ninaijua. Ninajua
jambo gani baya na jambo gani zuri.
Hata Nyerere aliiokosoa CCM
Alisema si dhambi kuikosoa CCM ikiwa tu dhamira inakuwa ni kuijenga na
kuiimarisha na kwamba hata Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alikuwa
akiikosoa.
“Mwaka 1995 wakati mwalimu anazunguka kumnadi (Benjamin) Mkapa alikuwa
anasema CCM kokoro hili limebeba watu wote kuna wengine humu nikijiuliza
inakuwaje tuko chama kimoja nao. Yalikuwa maneno makali. Alienda Musoma
pale akasema nyie CCM mmesimamisha mgombea wenu pale mla rushwa. Huyu
mimi sitampigia kura nitampigia yule wa NCCR-Mageuzi.”
“Hivi kuna maneno makali nimeyasema kuliko haya? Mwalimu alisema maneno
makali sana, lakini akasema kuna maneno ya uongo? Ni lazima tujenge
utamaduni wa kukosoana ili kujenga”
Mbunge huyo alitumia mahojiano hayo kumpongeza Rais Magufuli kwa
kutimiza miaka miwili madarakani, lakini akasema upo mjadala wa namna
anavyotekeleza ilani ya CCM.
Nape alisema yote yaliyoingizwa katika ilani ambayo Rais Magufuli
anaitekeleza kwa mafanikio, yalitokana na ziara yake yeye na Kinana
iliyowachukua miezi 36 ya kukiimarisha CCM.
“Tulipokuwa tunazunguka yapo mambo mengi tuliyasema. Yale ndiyo yalikuja
kuzaa ilani ya uchaguzi ya CCM (2015-2020). Yale ndio yalikuja kuzaa
mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
“Sasa hapa tunapotimiza miaka miwili, ukifanya tathmini mambo mengi
anayoyafanya Rais Magufuli pamoja na kumpongeza kwa kufikisha miaka
miwili, ni yale ambayo tuliyaweka kwenye ilani.”
Alisema walipozunguka mikoani, wananchi walilalamikia kuhusu kuporomoka
kwa nidhamu ya utumishi wa umma, wingi wa sherehe za kitaifa, mikataba
mibovu ya madini na rushwa.
“Shida ya nidhamu katika utumishi wa umma ilikuwa kubwa. Tuliikuta kila
mahali. Hili ni jambo moja Rais Magufuli amelisimamia vizuri,”alisema.
Aliyataja maeneo mengine ambayo alisema Rais ameyasimamia vizuri kuwa ni
kudhibiti matumizi ya Serikali, kusimamia sera ya uchumi wa viwanda na
kushughulikia migogoro ya ardhi.
Maeneo mengine ambayo alisema Rais amewafurahisha Watanzania ni kuondoa
utitiri wa kodi kwa wakulima, kudhibiti rasilimali ya madini na
kusimamia masilahi ya watumishi wa umma.
“Kwa hiyo amefanikiwa kugusa kila mahali lakini mjadala uliopo ni namna
anavyoyatekeleza haya mambo. Hapa ndipo palipo na mjadala na watu wengi
wanazungumza hapo.
“Hili mimi sitegemei watu wote watakubaliana. Wako wanaodhani angeenda
taratibu kidogo, wapo wanaodhani akaze zaidi, wapo wanaodhani afinye
zaidi na wako wanaodhani aende mdogomdogo.”
Nape alisema hakuna ubishi nchi ilikuwa katika matatizo makubwa ya
rushwa na watu walitamani kupata kiongozi ambaye hataona aibu hata
akimkuta rafiki yake anafanya ufisadi amshughulikie.
“Tunadhani Magufuli ameanza vizuri. Mjadala utakuja tu hivi katika
utekelezaji pengine tupunguze mwendo, twende kasi zaidi, tutumie busara
zaidi, tutumie upole fulani hivi. “Huu ndiyo mjadala ambao upo ambao
nadhani si mbaya lakini sio ambao unapaswa kumrudisha nyuma. Kwa
tathmini yangu mimi amefanikiwa kwa miaka hii miwili kutengeneza
mwelekeo fulani.”
“Kitakachofuata sasa hapa ni namna ya kuboresha utekelezaji wa yale
tulioyaweka kwenye ilani ya uchaguzi, yale ambayo ni matumaini ya
Watanzania na yale ambayo tuliwaahidi,” alisema.
Ajibu kauli ya Nyalandu CCM kupoteza mwelekeo
Akizungumzia kauli ya Nyalandu kuwa CCM imepoteza mwelekeo, Nape alisema
kwake anadhani huo ni mtizamo wake na wala hataki kupuuza mtizamo wake
huo wala kuubeza.
“Na mimi naamini CCM haijapoteza mwelekeo na mtakumbuka haya maneno
Nyalandu sio wa kwanza kuyasema. Aliwahi kuyasema Horace Kolimba miaka
hiyo na bado iko madarakani”
“Aliwai kusema Kingunge Ngombale Mwiru kuwa CCM imeishiwa pumzi na bado
inapumua. Haya maneno ni mitizamo ya watu na Nyalandu anayo haki ya kuwa
na mtizamo wake,”alisema.
“Alipotoka nilisema hivi kwamba aliibua hoja sita ukiacha hiyo ya
kupoteza mwelekeo. Nikasema hizi hoja zote alizoziibua zinazungumzika
ndani ya chama chetu. Angeweza tu kuzileta tukajadiliana”.
Kwa sababu ukisema CCM imepoteza mwelekeo ukaandika paper (mada) ukaja
nayo ndani vikao uka justify (ukaitetea) ndio njia bora ya kurekebisha
chama na sio kuondoka,”alisema na kuongeza;-
“Ndio maana alipoondoka mimi nika tweet nikasema kama yapo mapungufu ndani ya CCM nitayashughulikia nikiwa ndani ya CCM”
“Mimi katika utumishi wangu ndani ya CCM yako mengi sana ambayo
nimeyasukuma ndani ya chama na yametokea ikiwamo kuibadili kabisa ile
idara ya itikadi na uenezi”.
“Ninaamini katika kuleta mabadiliko. Kila mmoja kwenye nafasi aliyopewa
akijitahidi kuleta mabadiliko fulani CCM itabadilika. CCM ya leo sio CCM
ya jana”.
“Ndio maana kuna kauli mbiu CCM Mpya, Tanzania Mpya. Tunapotaka kuijenga
Tanzania mpya ni pamoja na fikra na mawazo. CCM mpaka leo haina mbadala
kwababu ya mfumo wake”.
Nape alisema Chadema wamejitahidi kujenga msingi chini lakini
wameshindwa na chama chao kimebaki ngazi ya kitaifa zaidi lakini CCM ina
uongozi hadi chini ngazi ya balozi na shina.
“Lakini CCM balozi wa nyumba kumi anajijua ni CCM na ndio nguvu ya CCM
ilipo. Hata uwezo wa kupanga. Ukitaka kuiua CCM lazima uue mfumo wake
jambo ambalo haliwezekaniki,”alisema.
“Kusema CCM inapoteza mwelekeo ghafla sio sawa lakini kusema hakuna
mapungufu nayo sio sawa. Yapo mapungufu yanashughulikiwa na yanaweza
kumalizwa na vikao na mfumo wa chama”
“Haya mapungufu ambayo pengine Lazaro aliyaona au wengine wanayaona dawa
sio kuyakimbia. Dawa ni kukaa kuyashughulikia. Wewe mwenzetu unayeona
yanakukera sana lete hoja”
Nape alitolea mfano walipoingia kuwa Katibu Mwenezi, kulikuwa na kitengo
cha propaganda kilichokuwa kikiongozwa na watu waliotoka upinzani
ambacho alitoa hoja kikabadilishwa.
“Hiki kitengo kilikuwa kinaongozwa na Tambwe Hiza. Moja ya jambo ambalo
lilikuwa linanikera sana ni kitengo hiki kuwa na historia ya kuongozwa
na watu waliotoka upinzani”
“Hili lilikuwa moja ya jambo lilikuwa linapeleka sura mbaya kule nje.
Nilipoenda nikasema lazima tutoe hii. Tukaondoa propaganda tukatengeneza
mawasiliano na umma”
“Tukaweka mawasiliano sio propaganda tu, kikaongozwa na Daniel Chongolo
kwa muda mrefu tu na akakijengea heshima kubwa sana na ndio hapo
tukarudisha mahusiano na vyombo vya habari”.
Nape alisisitiza kuwa endapo kuna mwana CCM anayeamini katika itikadi
yake anayaona mapungufu fulani, ongeza nguvu ya kuleta hoja za
mabadiliko ndani ya chama na sio kukimbia.
Chanzo: Mwananchi
0 Comments