SIRI YA LIPULI KUWAFUNGA SIMBA NA YANGA YAFICHUKA

KOCHA Msaidizi wa Lipuli FC, Selemani Matola, amefichua siri ya kikosi chao kutoa sare na timu kubwa za Simba, Yanga katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, kuwa ni malengo waliyoyaweka muda mrefu.

Katika mchezo na Simba juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Lipuli ilitoka sare ya bao 1-1, matokeo ambayo ni sawa na yale waliyotoka nayo Yanga katika mchezo wa kwanza wa ligi ulipigwa uwanjani hapo Agosti 27, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Matola alisema malengo waliyojiwekea yametimia kwa sababu walipanga kushinda au kutoka sare, pindi wanapokutana na timu hizo.

Alisema waliwaheshimu Simba kama timu kubwa iliyowekeza na yenye uwezo wa kucheza kuliko wao, lakini walihakikisha wanaweka ulinzi imara kuwazuia wasilete madhara kwenye goli lao.

“Tulichokifanya kwa Simba ndiyo kile kile cha Yanga na tumefanikiwa, maneno yalisemwa mengi kuwa tutawaachia, ni kweli mimi ni Simba hakuna asiyejua, nimecheza na kufundisha lakini hii ni kazi lazima niangalie kazi,” alisema Matola.

Kuhusu usajili alisema wanahitaji kuimarisha kikosi hicho kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, kwa kuongeza wachezaji zaidi ya wanne hasa eneo la ushambuliaji.

“Usajili wetu uliopita haukua mzuri kutokana na vurugu zilizokuwepo Iringa, hivyo kutulazimu kufanya kwa muda mfupi, ukiangalia kikosi chetu hakifungwi mabao mengi kwa kuwa tupo vizuri nyuma lakini mbele bado kunahitaji marekebisho,” alisema.

Post a Comment

0 Comments