HII NDIO MOTISHA KUBWA KWA WACHEZAJI WA KLABU YA SIMBA WANAOIPATA

SIMBA ndiyo timu yenye kikosi bora na cha gharama kubwa zaidi Ligi Kuu Bara msimu huu. Kwa mujibu wa Ofisa Habari wake, Haji Manara, thamani ya kikosi chao kinachoongoza msimamo kwa pointi 35, ni zaidi ya Sh1.3 bilioni.

Unafikiri hiyo ni habari kubwa sana? Hapana. Sikia hii. Simba ikishinda kila mechi moja, nyota wake hupewa cha Sh10 milioni ili wagawane ikiwa ni asante tu kwa furaha waliyopeleka Msimbazi. Pesa hiyo haina longolongo na hutolewa mara tu baada ya mchezo kumalizika. Achana na hilo pia.

Sasa habari kubwa zaidi ni kwamba katika mechi za duru la kwanza, Simba imeshinda michezo 10 kati ya 15, hivyo wachezaji wake kutia kibindoni kiasi cha Sh100 milioni ambazo wamegawana na ndizo zinawasaidia kufanya vurugu za manunuzi ya hapa na pale huku mtaani.

Habari njema zaidi ni kwamba Simba imetupia mabao 35 katika mechi hizo za mzunguko wa kwanza, hivyo kufanya thamani ya kila bao walilofunga kuwa Sh2.8 milioni. Hiyo ni kwa kugawanya posho ambazo wamevuna kwenye mechi hizo za duru la kwanza ambazo zimeiacha timu yao ikitanua kileleni.

Sasa kama ulikuwa hujui, wachezaji wa Simba wanapaswa kumpa heshima kubwa staa wao Emmanuel Okwi ambaye ndiye kinara wa mabao akiwa ameshafunga mara 12 katika duru la kwanza.

Mabao hayo ya Okwi yana thamani ya Sh34 milioni na ndiyo yaliyopeleka mkwanja mnene zaidi kwa nyota hao ambao wanaishi kistaa jijini Dar es Salaam.

Kiongozi wa wachezaji wa Simba uwanjani, John Bocco, naye amezidisha furaha Msimbazi kwa kufunga mabao saba ambayo kwa mujibu wa posho walizovuna kwenye duru hilo la kwanza yana thamani Sh20 milioni. Kichuya naye amewasaidia wachezaji wenzake kupata Sh17 milioni baada ya kufunga mabao sita kwenye duru hilo la kwanza.

KOTEI, GYAN WANENA
Akizungumzia uwepo wa posho katika mechi wanazoshinda, kiungo Mghana James Kotei, amesema viongozi wa timu hiyo waligundua itakuwa hamasa kwa wachezaji kufanya vizuri na kweli imeongeza morali ya kushinda kila mechi ndio maana wamepata matokeo hayo mazuri katika mzunguko wa kwanza.

“Kama unataka kupata faida katika biashara lazima kuwe na motisha kwa wafanyakazi wako, basi hata kwenye mpira unatakiwa kufanya hivyo ili kupata matunda ya uwekezaji ambao unafanyika katika klabu,” alisema Kotei.

Kwa upande wake nyota mwingine Mghana, Nicholas Gyan, alisema: “Kitu kizuri sana wanafanya viongozi wa Simba na inaongeza morali kwetu wachezaji kushindana kwa nguvu zaidi mwanzo mwisho ili kupata ushindi na kuipaisha zaidi klabu yetu.

Post a Comment

0 Comments