MIAKA 20 YANGA HIJAWAHI KUPATA USHINDI KATIKA UWANJA WA SAMORA IRINGA

Baada ya miaka 20, Yanga imepata ushindi wake wa kwanza kwenye Uwanja wa Samora kwa kuichapa Lipuli kwa mabao 2-0 mjini Iringa.

Tangu 1998, Yanga haikuwahi kushinda kwenye uwanja huo inapocheza dhidi ya Lipuli katika mechi za Ligi Kuu Bara wakifunga mara mbili na kupata sare mmoja kabla ya ushindi wa jana.

Mabao ya Papy Tshishimbi na Pius Buswita yalitosha kuipa Yanga ushindi muhimu na kurudisha kujiamini kwao wakielekea katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St. Louis ya Shelisheli Jumamosi ijayo.

Ushindi huo pia umeifanya Yanga kufikisha pointi 31 na kuisogelea Simba iliyo kileleni na pointi 35 ambayo leo inaikabili Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mabingwa watetezi Yanga ilianza mechi hiyo kwa utulivu wa hali juu na kuwaacha Lipuli watawale mchezo katika dakika 10 za mwanzo kwa mashambulizi yaliyokosa umakini.

Yanga ilipata pigo dakika 14, baada ya kipa wake namba moja Mcamerooni Youth Rostand kuumia na kutolewa nje akiwa kwenye machela na nafasi yake kuchukuliwa na chipukizi Ramadhan Kabwili.

Uzembe wa mabeki wa Lipuli katika kucheza mpira wa kona ulitoa mwanya kwa kiungo Kabamba Tshishimbi kufunga bao la kwanza kwa Yanga katika dakika ya 19 kwa shuti kali akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Lipuli, Aghaton Antony.

Antony alitema mpira wa kichwa uliopigwa na Emmanuel Martin aliyekuwa akimalizia kona iliyopigwa na Geofrey Mwashiuya.

Kipindi cha pili, Yanga ilipata bao la pili lililofungwa na Buswita akimalizia pasi ya Obrey Chirwa baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza katika dakika ya 55

Post a Comment

0 Comments