NYOTA 11 YANGA KUIKOSA NJOMBE MJI

Mabingwa watetezi Ligi Kuu Bara, Yanga itawakosa nyota wake 11 wa kikosi cha kwanza kesho Jumanne itakapoivaa Njombe Mji kwenye Uwanja wa Uhuru.

Kutokana na kuandamwa na majeruhi wengi katika kikosi cha kwanza mashabiki wa timu hiyo hivi sasa wameanza kuifananisha timu hiyo na hospitali ya Mloganzila walipoahamishiwa wagonjwa wa Muhimbili na kulazwa huko.

Tangu kuanza kwa msimu huu Yanga imekuwa katika wakati mgumu kutokana na wachezaji wake wengi kuumia mara kwa mara hivyo kupunguza ufanisi wa kiksoi hicho.

Daktari wa Yanga,Edward Bavu amethibitisha Yanga kuwakosa wachezaji 11 katika mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi

Wachezaji watakosekana ni kipa Youth Rostand,Juma Abdul, Ibrahim Ajib, Amiss Tambwe, Donald Ngoma, Andrew Vincent, Haji Mwinyi, Thaban Kamusoko, Abdallah Shaibu 'Ninja, Pato Ngonyani na Yohana Nkomola.

Rostand aliumia goti katika mchezo uliopita dhidi ya Njombe Mji hivyo hapana shaka mchezo wa kesho Ramadhan Kabwili ataanza akisaidiana na Beno Kakolanya.

Kocha msaidizi wa Yanga,Shadrack Nsajigwa'Fuso' alisema licha ya kwamba timu yake inapitia kipindi kigumu cha wachezaji wengi kuwa majeruhi lakini wataendelea kupambana ili kuhakikisha malengo yao yanatimia.

"Tangu mwanzo wa msimu tumekabiliwa na majeruhi ya mara kwa mara, lakini nashukuru wachezaji waliopo wanaendelea kupambana na kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri."

Faraja pekee kwa Yanga pamoja na kuandamwa na majeruhi bado wamefanikiwa kushinda michezo yake ya Ligi Kuu.

Yanga ilichapa Azam kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na mwishoni mwa wiki ilivunja mwiko kwa kuifunga Lipuli nyumbani kwao Iringa kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Samora.

Yanga ilifanya mazoezi yake ya mwisho jana asubuhi kwenye Uwanja wa Polisi, Kurasini kujiandaa na mechi yake dhidi ya Njombe Mji.

Wapinzani wao Njombe Mji wenyewe leo asubuhi ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru saa tatu asubuhi mpaka saa sita jua likiwa kali, lakini vijana wa Njombe hawakuonyesha kuchoka.

Mwanaspoti

Post a Comment

0 Comments