Wakati bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2022/23 ikitarajiwa kuwasilishwa bungeni wiki ijayo, wadau wa sekta ya usafirishaji nchini wameeleza matarajio yao katika mwaka ujao wa fedha, wakitaka kuwepo punguzo la bei mafuta na kodi.
Moja ya mambo wanayotarajia ni pamoja na kushuka kwa bei ya mafuta ambayo kwa namna nyingine imesababisha kupanda kwa bidhaa na huduma kama vile bei za vyakula, vifaa vya ujenzi na nauli za daladala na mabasi yaendayo mikoani.
Ongezeko la bei ya mafuta limetokana na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Russia ambazo ni wazalishaji wakubwa wa mafuta. Nchi hizo pia zinazalisha kwa wingi ngano, hivyo, vita hiyo imesababisha mtikisiko katika uchumi wa dunia.
Akizungumzia matarajio yao, Mkurugenzi wa mawasiliano wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo, alisema kitu kikubwa wanachotarajia ni Serikali kushusha bei ya mafuta.
“Sisi matarajio yetu ni mafuta yashuke, hali ya mafuta bado siyo nzuri. Kwa hiyo tunaiomba Serikali itenge bajeti ili kuangalia issue (suala) hii ya mafuta,” alisema.
Kuhusu kodi na tozo mbalimbali, Mwalongo alisema tayari walishawasilisha serikalini mapendekezo yao, hivyo wanasubiri kuona Serikali ikitekeleza kama ilivyowaahidi kuzitatua changamoto hizo.
Matarajio usafiri wa anga
Katika mwaka ujao wa fedha, sekta ya usafiri wa anga inatarajia angalau kuanzishwa kwa hatua zinazolenga kuongeza ukwasi wa mashirika ya ndege, watoa huduma za ardhini na waendeshaji wengine wa viwanja vya ndege.
Hatua hizo ni pamoja na msamaha wa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa ndege iliyokodishwa, sehemu za ndege, injini za ndege na matengenezo ya miamala ya ndani.
Orodha ya hatua hizo pia inajumuisha kufuta leseni ya biashara ya utalii Tanzania (Tala) ambayo kwa mwaka inafikia Dola za Marekani 5,000 kwa mashirika ya ndege ya nje na dola 2,000 kwa mashirika ya ndege ya ndani.
Kwa mara nyingine wadau wanatarajia Serikali itazingatia kuondoa malipo mara mbili ya mfuko wa mafunzo wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na mfuko wa ushuru wa kukuza ujuzi (SDL), pamoja na msamaha wa kodi kwenye vifaa vya kutunzia baridi kwa ajili ya bidhaa zinazoharibika.
Pamoja na hayo, wadau wa masuala ya usafiri wa anga wanatarajia kupitiwa upya kwa sera zisizo rafiki ambazo zinaelekeza kampuni tanzu malipo ya Capital Gain Tax (CGT) endapo kutakuwa na mabadiliko ya umiliki wa kampuni hiyo.
Katibu mtendaji wa Chama cha Waendesha Ndege Tanzania (Taoa), Lathifa Sykes alilieleza Mwananchi kuwa kodi ya ongezeko la thamani ( Vat), inafanya mauzo ya ndege, sehemu za ndege, injini za ndege au matengenezo ya ndege katika soko la ndani kuwa ghali zaidi kuliko soko la nje.
Alisema ilikuwa inakatisha tamaa maendeleo ya matengenezo au uuzaji wa ndege katika soko la ndani kwa sababu inafanya miamala kuwa ghali zaidi.
Kuhusu suala la Tala, Sykes alisema wahudumu wa anga hawatakiwi kulipa, kwa sababu wanafanya kazi chini ya Wizara ya Uchukuzi na wanapaswa kupata leseni ya biashara ya jumla na leseni ya huduma ya anga kwa kiwango cha dola 2,500.
Mfuko wa Mafunzo wa TCAA (kifungu cha 74 cha Sheria ya Usafiri wa Anga), inajumuisha malipo mara mbili ya mafunzo kwa sababu waendeshaji lazima pia walipe SDL.
“Ushuru mara mbili hufanya gharama za kufanya biashara kuwa kubwa na hivyo kufanya safari za ndege ndani ya Tanzania kuwa ghali kuliko kusafiri kwa ndege kwenda Uingereza,” alisema.
“Kwa hali ilivyo, ni matumaini yetu kwamba Serikali itafanya kitu ili angalau tupate chumba cha kupumulia.”
Ofisa mtendaji mkuu wa Kampuni ya Uendeshaji Mifumo ya Ardhini, Swissport Tanzania, Mrisho Yassin anatarajia kuwa Serikali itazingatia kutumia Capital Gain Tax (CGT) tu kwa mauzo ya moja kwa moja ya hisa au mali, na sio kwenye usajili wa hisa za shirika hilo nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 56 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004, iwapo kutakuwa na mabadiliko ya umiliki katika kampuni hodhi, basi itachukuliwa kuwa kulikuwa na mabadiliko ya umiliki katika kampuni tanzu, ingawa hakuna mabadiliko ya umiliki wa hisa yanayofanyika katika kampuni tanzu..
“Hii haikubaliki kwa sababu kwa sera ya sasa, wenye hisa wanaona kuwa ni ghali kupata biashara zinazofanya kazi nchini Tanzania,” alilalamika Yassin.
Alisema mabadiliko hayo yanapaswa kuathiri tu upatikanaji wa hisa kwa njia isiyo ya moja kwa moja pale ambapo kuna maslahi kwa Tanzania.
Kuhusu suala la vifaa vya kushughulikia chumba cha baridi, bosi huyo wa Swissport alisema kama vile vifaa vya chumba baridi, wahudumu wa ardhi wanapaswa kufurahia msamaha wa kodi pia.
“Kutosamehewa kodi, kunafanya uwekezaji katika chumba cha baridi kuwa ghali sana,” alisisitiza.
0 Comments