CHADEMA KUANZA KUWAJIBU KINA MDEE MAHAKAMANI

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema akiwa na Katibu wake, John Mnyika katika mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam

MAOMBI ya kuomba kibali cha kufungua kesi ya madai kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema, yaliyofunguliwa na wabunge viti maalum 19, wakiongozwa na Halima Mdee, yanaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Maombi hayo yanasikilizwa leo Alhamisi, tarehe 30 Juni 2022, mahakamani hapo mbele ya Jaji Mustafa Ismail, baada ya mawakili wa Chadema wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, kuondoa mapingamizi waliyoweka dhidi yake.

Mawakili wa Chadema wanatarajiwa kuwasilisha kiapo kinzani pamoja na kujibu hoja za maombi hayo ya Mdee na wenzake 18.

Mahakama hiyo mbele ya Jaji Ismail, imepanga kuyasikiliza maombi ya kina Mdee, kwa muda wa siku 14.

Katika maombi hayo, wajibu maombi ni Baraza la Wadhamini la Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, wamehudhuria mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

Mbali na Mdee, miongoni mwa waleta maombi wengine ni Nusrat Hanje, Hawa Mwaifunga, Agnesta Lambart, Grace Tendega, Jesca Kishoa, Esther Matiko na Ester Bulaya.

Wamefungua maombi hayo baada ya Baraza Kuu la Chadema mnamo Mei, 2022, kutupilia mbali rufaa walizofungua kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya Chama hicho kuwavua uanachama, kufuatia msimamo wao wa kukubali kuapishwa kuwa wabunge viti maalum, kinyume na msimamo wa Chadema.

Credit- Mwanahalisi online

Post a Comment

0 Comments