CHONGOLO AAGIZA VIBOKO WANAOSUMBUA WANANCHI WAVUNWE



Baada ya watu wawili kupoteza maisha kwa kuliwa na viboko wilayani Busega Mkoa wa Simiyu, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameahidi kushinikiza udhibiti wa wanyama hao wakali dhidi ya wananchi.


Katika ufafanuzi wake kuhusu vifo hivyo, leo Ijumaa Juni 3, 2022 Mkuu wa Wilaya hiyo, Gabriel Zacharia amesema watu hao wameuawa kati ya Januari na Mei, 2022 wakiwa ziwani Victoria kwa shughuli za uvuvi.

"Niliita mamlaka husika walikuja watu kutoka Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), wamepita maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye familia za wafiwa, pia wameeleza mpango wa kujenga kituo cha kudhibiti wanyama hao.

"Tukio la Mei huyu mvuvi aliamka asubuhi na kwenda ziwani, akiwa ziwani chombo chake kilipigwa na mauaji yalifanyikia humo, lakini sio nje ya maji," amesema.

Chimbuko la hoja hiyo ni malalamiko yaliyotolewa na Diwani wa Mwamanyiri wilayani humo, Timoth Mayala amesema tatizo hilo limekuwa kubwa na kwamba wanaomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kukabiliana nalo.

Akizungumzia hilo, Chongolo ameahidi kuzungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii (Dk Pindi Chana) achukue hatua stahiki na za haraka ikiwemo kuwavuna viboko hao.


"Mimi nitawaagiza waje waangalie viboko wanaowasumbua wananchi kama wamezidi sana wavunwe.

"Na mara nyingine wasiwavune na kupeleka nyama huko wanakotaka na ninyi muonje kweli au sio kweli? Kama wao wanakula tunavyopanda na sisi wakivunwa si tule nyama. Lakini msiwavune kabla ya vibali maana mtakuwa majangili," amesema.

Post a Comment

0 Comments