KISENA KUENDELEA KUSOTA, WENZAKE WATATU WAACHIWA HURU

Wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiwaachia huru washtakiwa watano akiwamo Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Usafirishaji wa Mabasi yaendayo haraka (Udart), Robert Kisena, mwekezaji huyo ameendelea kushikiliwa kutokana na kuwa na kesi mbili za Uhujumu Uchumi zenye jumla ya mashtaka 37, yakiwemo ya kutakatisha fedha na kuisabaishia Serikali hasara ya Sh5.2 bilioni.

Mbali na Kisena, Charles Newe naye ataendelea kubaki mahabusu kutokana na kosa hilo.

Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 15 likiwamo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh2 bilioni.

Mbali na Kisena, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 38/2019 ni mke wa Kisena, Florence Mashauri; Kulwa Kisena, raia wa China, Chen Shi na Charles Newe.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo leo Ijumaa Juni 3, 2022 chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (PA) Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kutokuwa na nia ya kuendelea kesi hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Takukuru, Pendo Temu kudai kuwa wamepewa maelekezo na DPP kuwa shauri hilo liondolewe mahakamani hapo baada ya DPP kutokuwa na nia ya kuendelea nalo.

Amedai shauri hilo ni la muda mrefu lakini rekodi inaaonyesha lilikuwa linafanyiwa upelelezi wakati kesi hiyo ipo mahakamani.

"Shauri hili bado uchunguzi ulikuwa unaendelea wakati lipo mahakamani hivyo DPP ameamua kuliondoa mahakamani hivyo naiomba mahakama hii izingatie hilo," amedai Temu.

Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko alidai mahakama hiyo inapotoa uamuzi wake iangalie historia ya kesi hiyo kwa sababu ipo mahakamani tangu mwaka 2019 ambapo hawajui wanapotoka nje wateja wake watakamatwa tena na kufunguliwa mashtaka kwa hakimu mwingine.

Nkoko ameiomba mahakama hiyo kabla haijatoa uamuzi wa kuliondoa shauri hilo ikae na isome vipengele vyote kama itashindikana wataenda Mahakama Kuu ili washtakiwa hao wapate haki yao.

"Kilichopo hapa washtakiwa wanawatoa halafu wanawakamata tena wakati kesi yao ipo mahakamani kwa muda mrefu utakuta mtu alishakaa miaka mitano, wanakamatwa tena tena wanakaa miaka mitano mingine jumla kumi kwenye hatua ya upelelezi hivyo naomba mahakama hii isome vipengele vyote ikishindikana tutaenda Mahakama Kuu na tukiona hakuna haki iliyofanywa tutaenda mahakama ya juu zaidi," amedai Nkoko.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Rita Tarimo alisema amesikiliza hoja zilizotolewa pande zote mbili hivyo kutokana na mazingira hayo kesi hiyo inaondolewa kwa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (PA) Sura ya 20 iliyofanywa marekebisho mwaka 2019.

Tarimo amesema kama washtakiwa hao watarudishwa mahakamani hapo upande wa mashtaka wawe wamekamilisha upelelezi wao.

"Kama hamjakamilisha upelelezi msiwakamate, waendelee na upelelezi huku wapewe dhamana mkikamilisha upelelezi wenu ndio muwalete mahakani” amesema Tarimo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2011 na Mei 31, 2018 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu.

Katika shtaka la pili, Kisena, Kulwa, Simon na Florence wanadaiwa kujenga kituo cha mafuta ya petroli bila kibali kutoka Ewura.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Januari Mosi mwaka 2015 na Desemba 31, 2017 ambapo inadaiwa walijenga kituo hicho eneo la Jangwani bila kibali cha Ewura.

Pia, wanadaiwa kuisabishia hasara UDART ya Sh 2 bilioni.

Chanzo - Mwananchi

Post a Comment

0 Comments