POLISI WAWILI WASHIKILIWA KWA TUHUMA YA KUSABABISHA MAUAJI YA NG'OMBE MOROGORO











Polisi wawili wakamatwa wakituhumiwa mauaji Moro
FRIDAY JUNE 03 2022


 Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia askari wawili wa Kituo cha Polisi Mvua kwa tuhuma za kusababisha mauaji ya mkazi wa Mvuha Wilaya ya Morogoro, Hamis Hassan (30) maarufu Ng’ombe, baada ya kumpiga risasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro (RPC), Fortunatus Muslim amesema hayo leo Ijumaa Juni 3, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari juu tukio la mauaji lilitokea Mei 31 mwaka huu katika Kijiji cha Bwila Juu Kata ya Selembala wilayani Morogoro.

Kamanda Muslim amesema Mei 30 Scholastaica Mathias (29) mfamasia alifika katika kituo hicho cha polisi kutoa taarifa kuwa shamba lake alilolima ufuta limehairibiwa kwa kufyekwa na Hamis Hassan.

Amesema kuwa mtoa taarifa na mtuhumiwa walikuwa na mahusiano ya kimapenzi na katika mahusiano yao mtuhumiwa alitoa Sh100,000 ili kukodisha shamba na kulima ufuta.

“Baada ya ufuta huo kulimwa mahusiano ya wawili hao yalivunjika na kuanza kugombea mazao hayo,” ameeleza Kamanda Muslim.

Amesema wapenzi hao walifikishana ngazi mbalimbali za uongozi wa kijiji na kata kwa nia ya kupata suluhu lakini haikuzaa matunda na ndipo mtoa taarifa alipoamua kwenda kituo cha polisi na kufunguliwa kesi ya kuharibiwa mali.ADVERTISEMENT


Amesema baada ya hapo mkuu wa kituo cha polisi aliwatuma askari wawili kwenda kumkamata Hassan na askari walipofika eneo alipo mtoa taarifa walikwenda kuripoti kwa mtendaji wa kata, ambapo askari mmoja alikuwa amebeba silaha aina ya AK47.

“Mmoja alishuka kwenye pikipiki na kuzunguka nyuma ya nyumba yenye duka huku mwingine na mtendaji wakiwa wamebaki lakini baada ya muda kodogo walisikia milio ya risasi na kwenda kuona kilichotokea na kukuta Hamis amelala chini akiugulia maumivu”.

Kamanda amesema kuwa Hamis alifikishwa hospitali na kuanza kupata matibabu na alifariki baadaye kutokana na kuvuja kwa damu nyingi.

Amesema mwili ulifanyiwa uchunguzi wa daktari na mazishi tayari yamefanyika huku askari hao wakishikiliwa kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu matukio yanayojitokeza ya mauaji mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Zainabu Ally aliiomba Serikali kuhakikisha inawachukulia hatua wale wanaobainika kufanya mauaji kwa maksudi.
Chanzo - Mwananchi

Post a Comment

0 Comments