TUNDU LISSU NA LEMA WACHOCHEA MADAI YA KATIBA MPYA

Wakati Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwahamasisha wanachama wa chama hicho kuendelea kudai Katiba mpya, Mwenyekiti Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema yuko mbioni kurudi nchini kutokea Canada kuendeleza mapambano hayo.

Akihutubia wanachama wa Kanda ya Kaskazini kupitia mtandao wa Zoom uliofanyika katika ukumbi wa Shaaban Robert jijini Tanga leo Juni 4, Lissu anayeishi nchini Ubeligiji amesema, kisheria Katiba iliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Jaji Joseph Warioba muda wake umeisha.

Katika kufikia hatua ya kupata katiba mpya, amewaomba Watanzania kuungana mijini na vijijni kuwa sauti moja itakayowezesha mchakato wa katiba mpya kufikia.

"Mchakato huu si wa viongozi wa Chadema au CCM pekee bali unahitaji kuwa na nguvu ya umma ya pamoja kwa," alisema Lissu.

Kuhusu kurejea kwake Tanzania, amesema kwa kuwa kilichomkimbiza nchini ni suala la usalama wake ikiwamo kupigwa risasi na kunusurika kukamatwa mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2022, bado anasubiri mazingira ya usalama wake yawekwe.

"Nina imani kwamba mazingira ya mimi kurejea Tanzania yatakuwa mazuri kwa sababu hata mazungumzo yanayoendelea baina yetu na Serikali sehemu nyingine yanahusu hilo.

“Yakiwa mazuri nitarejea haraka kwa sababu kutoka huku na Tanzania ni saa chache," amesema Lissu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema ambaye pia alikimbilia nchini Canada baada ya uchaguzi mkuu wa 2020, amesema yuko mbioni kurejea.

"Ninaposikia wakimbizi nafika mbali sana kwa sababu mimi ni miongoni mwa walioonja machungu ya ukimbizi, hakuna kitu kizuri kama kuishi nchini kwako," amesema Lema.

Hata hivyo, Lema amesema yupo katika mchakato wa kurejea Tanzania baada ya kuridhishwa na mazingira ya usalama yaliyowekwa.

"Nimeshazigawa hata nguo zangu za baridi ya huku Ulaya, narejea Tanzania na sitarejea kinyonge. Nakuja na nguvu mpya ya kupambana," amesema Lema.

Amewaomba Watanzania kuungana kupigania njia sahihi ya utawala bora kwa kupata katiba itakayomuwajibisha yeyote atakayefanya makosa.

Katika Kongamano hilo ambalo lililohudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanga, Benson Kigaila, aliyekuwa Diwani wa kata ya Mwanzange kupitia CUF na baadaye kuhamia ACT Wazalendo, Rashid Jumbe amejiunga na Chadema akisema sababu iliyomvuta ni harakati za kweli za kudai katiba mpya.

“Nimekuja Chadema na kundi kubwa la waliokuwa wanachama wa ACT Wazalendo, hatukuja kutaka uongozi bali kuimarisha mapambano ya katiba mpya,” amesema Jumbe ambaye ni mwanasiasa mkubwa jijini Tanga.

Post a Comment

0 Comments