MSUVA AWEKA WAZI KUWA ANASAJILIWA YANGA AMA SIMBA


Aliyewahi kuichezea klabu ya Yanga Simon Msuva ameweka wazi kuwa ni timu gani atachezea hapa Bongo kati ya Simba ama Yanga. Kauli hii Msuva ameitoa wakati kuna habari nyingi mitandaoni wengine wakihusisha kuwa atasajiliw Yanga ama Simba.

Msuva anasema matamanio yake kwa sasa ni kucheza soka nje ya nchi ili kupata pesa nyingi kwa sababu familia yote inamuangalia yeye.

“Kwanza sitaki kusikia habari za klabu bingwa Afrika kwani kama nimeshindwa kuchukua kombe au kuvaa medali nikiwa Wydad siwezi kuvaa sehemu nyingine yoyote tena."

“Malengo yangu hivi sasa ni kupata pesa nyingi ya mpira, nahitaji kufaidika na kuna nchi ambazo nimezilenga kama Qatar, Saudi Arabia, Dubai, hizi ndio nataka kucheza hata kama watu wataongea kuwa huyu hana akili kwa nini kaenda huko bora angeenda Ulaya, sijali wala nini kila mtu na maisha yake."

Msuva na anaongeza; “Kama itatokea nafasi ya kwenda Ulaya nitakwenda ila nchi hizo zilizozitaja ndio kipaumbele changu cha kwanza kwani naamini nitapata hela na mpira nitacheza"

“Ujue Ulaya inawezekana hela ipo lakini sio hela ninayoitaka mimi lakini pia ukizingatia na pasipoti yangu inavyosema. Ujue mimi sina miaka 20, Ulaya inahitaji muda, kwa sasa kidogo umri umesogea hivyo lazima niwe na malengo nipate sehemu ambayo itakidhi mahitaji yangu maisha yangu kwani mwisho wa siku watu wataangalia maisha yako yakoje na hawatangalia historia yako kwamba umecheza Ulaya au wapi, ingawa historia ni nzuri kwenye maisha ila historia bila hela si chochote, “anasema Msuva.

Msuva anasema klabu zote mbili zilihitaji huduma yake ikiwemo na Azam lakini ameshawaambia kuwa kwa sasa hana malengo ya kucheza soka Tanzania. “Labda siku zijazo naweza kurudi kucheza soka Tanzania na kumalizia soka langu kwenye nchi yangu lakini kwa sasa chaguo langu la kwanza hadi la tatu ni kucheza nje ya nchi”.

“Ikitokea nikacheza Bongo kwa sasa labda machaguo yangu yote matatu yafeli lakini nina ofa saba hadi nane, za Ulaya mbili na tano za nchi za Uarabuni ila siwezi kutaja klabu hadi hapo dili litakapokamilika ndio nitataja naenda wapi.”

Post a Comment

0 Comments