MWANAFUNZI MZUNGU AKOJOLEA MALI ZA WANAFUNZI WEUSI AFRIKA KUSINI, AFUKUZWA CHUO


Chuo kikuu cha Afrika Kusini cha Stellenbosch kimemfukuza mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyenaswa kwenye video akikojolea mali za mwanafunzi mweusi.

Mwanafunzi huyo alifukuzwa chuoni kufuatia tukio lililoshukiwa kuwa ni la ubaguzi wa rangi huku chuo kikianzisha uchunguzi kuhusu suala hilo.

Wanafunzi kadhaa walifanya maandamano wakitaka hatua ichukuliwe dhidi yake .

Chuo kikuu kiliendesha uchunguzi wa kinidhamu kuanzia tarehe 15 Mei, na kuukamilisha tarehe 23 Juni.

Alhamisi, kamati kuu ya nidhamu ya chuo (CDC) ilimpata na hatia mwanafunzi kwa kukiuka sheria za nidhamu.

“Matokeo ya uchunguzi yalipelekea CDC kubaini kwamba hapakuwa na njia mbadala ila kumfukuza mwanafunzi mara moja katika chuo hicho.

Mwanafunzi huyo ana siku tano za kukata rufaa dhidi ya uamuzi.

Akizungumzia kuhusu matokeo ya uchunguzi Naibu Kansela wa Chuo hicho, Profesa Deresh Ramjugernath, alisema kuwa chuo kikuu kinaliangalia suala hilo katika “umakini mkubwa”.

“Chuo kikuu hakivumilii ubaguzi wa rangi, ubaguzi, na mienendo inayokiuka utu wa mtu mwingine ,” alisema.

Post a Comment

0 Comments