Hata hivyo, katika maandalizi ya mchezo huo, leo itaikaribisha KMC FC kwenye mechi ya kirafiki itakayopigwa kambini kwa Yanga, Avic Town iliyoko Kigamboni, Dar es Salaam.
Yanga ambayo inaendelea na maandalizi ya msimu mpya wa 2022/23 unaotarajiwa kuanza Agosti 17, mwaka huu, pia itafungua msimu mpya wa ligi hiyo kwa kucheza dhidi ya watani wao, Simba kwenye mechi ya Ngao ya Jamii ikitakayochezwa Agosti 13 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akizungumza na Nipashe jana, Daktari wa Yanga, Shecky Mngazija alisema kikosi chao kinatarajia kujipima na KMC katika Uwanja wa Avic Town leo wakijiandaa na kilele cha Siku ya Mwananchi na kwamba Kocha Nasreddine Nabi atautumia mchezo huo kuendelea kuwapima wachezaji wake wapya.
“Leo (jana) kikosi kimefanya mazoezi ya gym kwa ajili ya wachezaji kujiweka fiti, ikiwa ni maandalizi ya mechi ya kirafiki dhidi ya KMC, mchezo tunaotarajia kuchezwa katika uwanja wa kambi yetu ya Avic Town saa 10.30 jioni.
“Maandalizi yanakwenda vema na lengo la kucheza mechi za kirafiki ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo wetu wa Wiki ya Mwananchi dhidi ya Vipers,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais wa Klabu ya Yanga Hersi Said, jana amekabidhi vifaa mbalimbali vya shule katika Sekondari ya Jangwani pamoja na taulo za kike ikiwa ni mwendelezo wa kuisaidia jamii kuelekea kilele cha Siku ya Mwananchi.
Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo, Hersi alisema ametoa vifaa hivyo kutokana na kutambua umuhimu wa elimu.
"Huu ni mwendelezo wa wiki yetu ya Mwananchi ndio maana tumeamua kutoa vifaa hivi kwa wanafunzi pamoja na vifaa vya walimu," alisema.
Alisema leo kutakuwa na mbio za CRDB ambazo zitakuwa mahususi kwa wanawake wajawazito pamoja na watoto wenye matatizo ya moyo.
Mbali na hayo Alhamisi watakuwa na zoezi la kuchangia damu wakishirikiana na mdhamini wao mkuu SportPesa, ambalo litafanyika makao makuu ili kuisaidia Hospitali ya Taifa Muhimbili huku Ijumaa ikiwa ni dua kabla ya Jumamosi kuhitimisha kilele hicho Uwanja wa Mkapa.
0 Comments