Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko amesema Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ina upungufu mkubwa wa walimu hasa walimu wa kiume hivyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo.
Masumbuko ametoa ombi hilo leo Jumatano Agosti 9,2023 wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Shinyanga kilichokuwa na ajenda ya kupokea taarifa ya Utekelezaji wa shughuli mbalimbali kutoka katika kata kwa robo ya nne yam waka 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
“Manispaa yetu ina upungufu mkubwa wa walimu hasa walimu wa kike, unakuta kuna shule ina walimu 13 lakini mwalimu wa kiume mmoja pekee. Tunaomba kuongezewa walimu na kuwe na uwiano wa walimu wa kiume na wa kike kwani wanafunzi wa kiume wana mahitaji mengine yanapaswa kusikilizwa na walimu wa kiume na wanafunzi wa kike nao wanahitaji kusikilizwa na walimu kike”,amesema Meya huyo wa Manispaa ya Shinyanga.
“Polisi tunaomba bodaboda wanaopakia mbao mchukue hatua kwa sababu kuna malalamiko pikipiki zinachukua nafasi kubwa sana barabarani lakini zinabeba mzigo mkubwa juu ya kiwango kinachotakiwa”,amesema Masumbuko.
Kuhusu malalamiko ya wananchi yaliyowasilishwa na Diwani wa kata ya Mwamalili James Matinde juu ya kukosekana kwa huduma ya Umeme kwenye kata yote, Meya huyo amesema suaala hilo linashughulikiwa , Mkandarasi amepatikana na hivi karibuni huduma ya umeme itapelekwa kwenye vijiji vyote vitatu vya kata hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Said Kitinga amewataka Madiwani kutilia mkazo suala la Lishe shuleni huku akihamasisha ujenzi wa vyoo kwenye baadhi ya shule ikiwemo shule ya Sekondari Uzogore zenye upungufu wa matundu ya vyoo kwani kukosekana kwa vyoo kunafanya utu ukosekane.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga ambaye ni Mwanasheria Dorice Dario amesema juhudi za serikali zinafanyika ili kuweza kupata watumishi wakiwemo maafisa watendaji na suala la shule ikiwemo Uzogore Sekondari linashughulikiwa haraka na liliwekwa kwenye mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha huu.
Licha ya mafanikio yaliyofikiwa kupitia kikao hicho, Madiwani wamezitaja miongoni mwa changamoto zilizopo ni upungufu wa madarasa, uhaba wa matundu ya vyoo, kukosekana kwa huduma ya maji katika baadhi ya shule, upungufu wa maafisa watendaji ,ukosefu wa umeme kwenye baadhi ya maeneo mfano kata ya Mwamalili ambayo vijiji vyote havina umeme na upungufu wa walimu kwenye baadhi ya shule.

















































0 Comments