Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro.
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mkazi wa Kimara Temboni, Mtaa wa Amani, Selemani Haruna, maarufu Kwata (24), kwa tuhuma za kumuua msichana wa kazi za ndani, Editha Charles (22) na kuuficha mwili katika stoo ya vifaa vya ujenzi katika nyumba ya Agatha Stanslaus.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini hapa jana, alisema uchunguzi wa awali umeonyesha Julai 6 mwaka huu, majira ya asubuhi, mtuhumiwa alifika kwenye nyumba aliyokuwa anaishi binti huyo wa kazi, akijifanya fundi wa umeme na alitakiwa kuweka balbu.
"Alipoingia ndani, alimshambulia kwa kitu chenye ncha kali binti huyo na kumuua halafu akavunja chumba cha mwenye nyumba na kuiba Sh. milioni 1.8 na kutoweka.
"Polisi kwa kutumia wataalamu wake wa uchunguzi wa kisayansi na vyanzo vingine vya kiuchunguzi, walibaini mtuhumiwa huyo kuwa aliingia kwenye nyumba hiyo na kukaa kwa saa kadhaa na kutoka.
"Baada ya kumkamata na kumhoji kwa kina, alikiri kumuua binti huyo, kuvunja mlango wa chumba na kuiba fedha hizo na mwili wa marehemu aliuficha kwenye stoo ya nyumba hiyo huku akiwa ameufunika na vifaa mbalimbali vya ujenzi ili usionekane," alisema.
Kamanda Muliro alisema mtuhumiwa huyo ameonyesha kiasi cha fedha alizoziiba eneo hilo na zingine alidai mara baada ya tukio, siku iliyofuata alinunua vitu mbalimbali zikiwamo simu mpya aina ya Infinix, viatu vya mpira jozi mbili na begi la mgongoni lenye nguo mbalimbali mpya ambavyo navyo vimepatikana.
Kamanda Muliro alisema kitendo alichofanya mtuhumiwa ni cha kikatili na uchunguzi wa shauri hilo unakamilishwa ili afikishwe mahakamani.
Katika tukio lingine, Kamanda Muliro alisema Jeshi la Polisi linamshikilia Jonas Ziganyige (71) ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na mkazi wa Mbezi Juu kwa tuhuma za kumpiga risasi na kumuua Patient Romwadi (48), mfanyabiashara na mkazi wa Wazo Mivumoni, Kinondoni.
"Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Julai 9 mwaka huu, majira ya saa nne asubuhi, Recy Renso (52), mkazi wa Posta alifika eneo hilo na mtu huyo ambaye ni marehemu kwa sasa kwa lengo la kuangalia mipaka ya kiwanja chake.
"Mtuhumiwa alitoka ndani huku akionyesha kukasirishwa na hatua ya watu hao, akachukua bunduki na kumpiga risasi Patient Romward ambaye baadaye alifariki dunia.
"Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia lakini upelelezi ulifanywa haraka na Julai 10 mwaka huu alikamatwa eneo la Kibaha Maili Moja akiwa amejificha," alisema.
Kamanda Muliro alisema Jeshi la Polisi limeipata silaha aliyotumia mtuhumiwa ambayo ni aina ya Mark IV ikiwa na risasi nne
"Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kujibu mashtaka yanayomkabili. Jeshi la Polisi linaendelea pia na jitihada za kuzuia vitendo vya kihalifu kwa kufanya operesheni kali inayoongozwa na taarifa fiche dhidi ya uhalifu na wahalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
"Watuhumiwa wanane sugu wa uvunjaji nyumba na kuiba vifaa vya magari akiwamo Jumanne Omary (28), mkazi wa Mikwambe na wenzake saba, wamekamatwa wakiwa na Tv flat screen nne za aina ya mbalimbali, kompyuta mpakato mbili, sabufa moja, simu aina mbalimbali tano pamoja na vifaa vya kutendea uhalifu vikiwamo mikasi miwili mikubwa ya kuvunjia, panga moja, kisu kimoja, prize na bisibisi, tochi na nyaraka mbalimbali.
Pia alisema wamekamata gari lenye namba za usajili T 787 DGW aina ya Toyota Gaia, likihusishwa na kutumiwa kwenye vitendo vya kihalifu.
"Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwani kwa kufanya vitendo hivyo watakamatwa na watajikuta wakiwa katika msuguano mkali wa kisheria na vyombo vya dola," alisema.
Na IPP MEDIA
0 Comments