MAYELE AANDALIWA MIAKA MIWILI YANGA


Fiston Mayele.

UONGOZI wa Yanga umepanga kuanza haraka mazungumzo ya kuongeza mkataba wa miaka miwili na mshambuliaji wao, Fiston Mayele, kwa lengo la kuendelea kuimarisha kikosi cha timu hiyo kwa misimu ijayo ya mashindano.

Mayele anatarajiwa kuwasili nchini muda wowote kuanzia sasa tayari kwa kujiunga na wenzake kwenye kambi ya Avic Town kule Kigamboni, Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari, tayari uongozi huo umeshaandaa mkataba na sasa anasubiriwa nyota huyo kwa ajili ya mazungumzo na kuelewana katika maslahi.

Chanzo hicho kimepasha kwamba, Mayele amebakiza mkataba wa mwaka mmoja ambao unafikia tamati msimu ujao na sasa wanajiweka katika mazingira mazuri kuendelea kubaki nae kwa miaka miwili zaidi.

"Mayele ana mkataba wa mwaka mmoja, lakini bado tunahitaji huduma yake, sasa tumeanza mazungumzo ya kutaka kumwongezea mkataba mwingine wa miaka miwili," kilisema chanzo hicho.

Hivi karibuni Rais wa Yanga, Hersi Said alisema Mayele bado yuko katika mipango yao na ana mkataba wa mwaka mmoja unaotarajiwa kufikia tamati msimu ujao, lakini wako mbioni kumwongezea mwingine.

Alisema kulingana na mahitaji ya kikosi chao na mipango ya benchi la ufundi la timu hiyo inayoongozwa na Kocha Nesreddine Nabi, mshambuliaji huyo yuko katika mipango na wako katika hatua za kumwongezea mkataba mwingine.

"Suala la kuuza mchezaji kwa sasa halipo, kuhusu Mayele bado yuko Yanga na ataendelea kuwapo, kwa sasa malengo yetu ni kuimarisha timu yetu kufikia malengo ya kutetea mataji yetu yote matatu kwa msimu ujao, lakini kufanya vizuri zaidi michuano ya kimataifa," alisema Rais huyo.

Naye Mwakilishi wa Meneja wa Mayele, Nestory Mutuale, alithibitisha kuwepo mazungumzo hayo na kudai kwamba, kwa sasa Yanga hawana mpango wa kumwachia mchezaji huyo.

“Mayele anatarajia kurejea nchini muda wowote kuanzia sasa na kuhusu kuondoka Yanga ni ngumu kwa sababu hawataki kumwachia na sasa wameanza mazungumzo kwa ajili ya kuongeza mkataba wa miaka miwili,” alisema Matuale.

Post a Comment

0 Comments