TANZANIA YAGUNDUA PANYA WENYE UWEZO WA MAAJABU


TANZANIA imeishangaza dunia baada ya kufanikiwa kugundua na kuwafundisha panya tisa wenye uwezo wa kuokoa, kutambua majeruhi na watu waliopoteza maisha katika majengo yaliyoharibika kutokana na kuanguka au tetemeko la ardhi

Wakati huo huo, jopo la wanasayansi na watafiti wa panya kutoka nchi zaidi ya 50 duniani, wanakutana kwa siku nne jijini Arusha kujadili udhibiti, baiolojia na njia za kisayansi, zinazopaswa kutumika kutatua matatizo yanayotokana na panya.

Mwenyekiti wa mkutano huo, ambaye ni Mtaalamu wa Utafiti wa ikolojia ya panya kutoka Kituo cha Umahiri cha Utafiti wa Panya cha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Rhodes Makundi alisema: “Watafiti hawa wanaangalia mambo tofauti, kwanza wanaangalia kitu kinachoitwa taxonomy (utambuzi panya wako wa aina gani).

“Pili wanaangalia biodiversity (katika mazingira wanayoishi, kwamba kuna wanyama gani na wanahusianaje), kingine ni juu ya magonjwa yanayotukabili kutokana na panya, kwa mfano kugundua tauni na kifua kikuu”.

Alisema: “Pia, tunaangalia udhibiti wa panya, kwa kutumia njia za kiikolojia, tunaangalia tabia za panya, tunaangalia panya wanaopatikana katika milima na mabonde katika Afrika, hasa katika nchi za Afrika ya Mashariki”.

Zaidi aliongeza: “Na kingine ni kuangalia matumizi ya panya ili kuleta faida kwa jamii; kwa mfano matumizi ya panya kwenye kugundua mabomu, kugundua ugonjwa wa tauni na mambo mengine, ambayo panya anaweza akatumika.”

Prof. Makundi, alisema baada ya mkutano huo wanatarajia, jopo la wanasayansi hao ambao wamefanya utafiti kwenye nchi tofauti, hasa kudhibiti panya, wanasayansi wa Tanzania, watajifunza mambo yanayofanyika mahali pengine, pale inapowezekana utaalamu huo watauchukua kuutumia hapa nchini kutatua matatizo ya panya.

Alisema: “Kwa mfano, utafiti wa matumizi ya panya kwenye kugundua kutegua mabomu, kugundua magonjwa ya tauni. Unaweza kuona utafiti huo unatumika nchi nyingi kama Cambodia huko.

“Kimsingi, huu ni mkutano ambao una manufaa kwa kila anayeshiriki na jinsi anavyoweza kuutumia katika nchi yake, lakini kubwa kabisa ni ugunduzi mwingi wa kisayansi.”

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, alisisitiza kuwa kwa sasa umefika wakati, wanasayansi na watafiti hao, kutoka hadharani kuelezea zaidi faida ya eneo hilo ili lisibaki tu kuwa eneo la utafiti.

Mtafiti kutoka Shirika la Uhisani la APOPO linalojishughulisha na maisha ya panya, lililoko chini ya Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), Venance Kiria, alisema shirika hilo limewafundisha panya tisa wa uokozi, ambao mpaka sasa wako kwenye hatua ya mwisho katika ufundishaji.

Alisema: “Hivi sasa panya hao wa Tanzania, wana uwezo wa kutafuta mtu akiwa umbali mrefu, lakini siyo kwa kiwango kile ambacho tunakitaka, hasa kwenye majengo yaliyopata ajali”.

Post a Comment

0 Comments