WATU WATATU WAFARIKI KWA KUPIGWA RADI GEITA

WATU watatu wa familia moja wakazi wa kitongoji cha Idoselo, Kijiji cha Kasesa, Busanda wilayani Geita mkoani hapa, wamefariki dunia kwa kupigwa na radi, huku mwenzao mmoja akijeruhiwa katika tukio hilo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Idoselo, Jackson Mchele akizungumuza leo katika mazishi ya watu hao, amewataja waliofariki ni bibi wa familia, Mageni Nkoma (75), mama wa familia, Maleciana Ludewa (57) na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, Kelvin Shadrack.

Amesema taarifa za tukio hilo alizipata muda mchache baada ya mvua kukatika, ambapo walifanya mawasiliano na viongozi wa juu na kisha madaktari kwa ajili ya kufanya vipimo kama watu hao bado wana uhai.

“Nilipopata taarifa, nikafika kushuhudia tukio, nikakuta watu hao watatu wameshazimia, tukaanza kuchukua hatua, ili kuwaokoa. Madaktari walikuja majira ya saa moja usiku kuwapima hawa waliozimia, kumbe wamefariki,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasesa, Zacharia Lucas, amesema tukio kama hilo ni mara ya kwanza kutokea tangu aingie madarakani, ikiwa ni miaka nane sasa na kuwaomba wananchi kuwa watulivu na kuachana na imani potofu.

Baba wa familia hiyo, James Lubiyu amesema tukio hilo wakati linatokea, marehemu walikuwa ndani ya nyumba wamejikinga na mvua, huku yeye pia akiwa ndani na radi ilipotokea athari zilianza kuonekana kwenye miti.

Akithibitisha tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amesema baada ya kupata taarifa, serikali imeshiriki kwa kutoa rambirambi ya majeneza na kusimamia mazishi.

Post a Comment

0 Comments